Usajili wa kimkakati...Mastaa 13 kutua Simba

Usajili wa kimkakati...Mastaa 13 kutua Simba

BAADA ya kuona kuna kila dalili ya kushindwa kutetea mataji yao msimu huu, Simba imeanza usajili wa kimkakati. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba mezani kuna orodha ya wachezaji 13 wapya wote raia wa kigeni.

Kwenye orodha hiyo mpya kuna washambuliaji watatu, viungo wako saba na mabeki wa kati watatu. Lakini uhakika ni kwamba kwenye mlolongo huo watachujwa na kubaki watano tu wa maana yaani washambuliaji wawili, viungo wawili na beki wa kati mmoja wa kuanza na Enock Inonga endapo Joash Onyango atazingua kuongeza mkataba mpya.

Twende pamoja. Kwenye kiungo mkabaji kuna Lamine Camara(Msenegali), Alwyn Tera(Mkenya) wote kutoka Generation Footbal ya Senegal na Martial Zemba Ikoung(Mcameroon) anayechezea Apejes FC ya Cameroon.

Wakati nafasi ya beki wa kati majina matatu yaliyopendekezwa ni Solomon Sakala (Zambia), Carof Bakoua (RD Congo) wote kutoka Zesco United ya Zambia na Soleyman Sakande (Burkina Fasso) anayekipiga kwenye timu ya AS Otoho d’Oyo kutoka nchini Congo.

Katika mapendekezo mengine ya benchi la ufundi nafasi ya ushambuliaji chaguo la kwanza ni Moses Phiri (Zambia) ambaye tayari usajili wake ndani ya kikosi hicho umekamilika na imebaki utambulisho tu.

Kwenye nafasi hiyo pia wamependekezwa Frank Mbela Etouga (Cameroon) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Cesar Manzoki (DR Congo) wa Vipers FC ya Uganda. Manzoki naye dili lake limeshakamilika anasubiri tu kusaini mkataba kwani mambo mengi wameshakubaliana. Mwanaspoti limejiridhisha pia katika mapendekezo hayo ya Simba mpya yumo, Victorien Adebayor (Niger) ambaye tayari dili lake limeshashindikana baada ya kusaini RS Berkane.

Aziz Ki (Burkina Fasso) dili lake limeshashindikana Simba na anahusishwa na kujiunga na Yanga na inadaiwa pia Zamalek ya Misri wameingia kati lakini makocha wa Yanga wamemuahidi kumpa muda mwingi wa kutumika.

Moryale Sylla(Guinea) wa Horoya yeye bado dili lake linaendelea kama tulivyokujuza kwenye toleo la jana. Mwanaspoti linajua Simba kwasasa imeweka pembeni kamati yake ya usajili na Barbara Gonzalez ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ ndio wanaosimamia mchakato huo wa usajili wa Simba mpya. Try Again alisema hivikaribuni kuwa baada ya kushindwa kufikia malengo yao msimu huu wao kama viongozi wamekutana na kubaini wapi wamekosea.

“Tumejua wapi tulikosea tunajipanga upya kwa msimu ujao, nilikutana na Rais wa heshima, Mohammed Dewji ‘MO’ amerudi atafanya usajili mkubwa hivyo kikubwa mashabiki wetu waendelee kutusapoti na wasikate tamaa,” alisema. Usajili wa Ligi Kuu Bara unaanza rasmi Julai 15.