Tiketi Simba, Yanga kuuzwa kwa namba ya viti

Muktasari:

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa tiketi anayonunua shabiki kufanana na namba ya kiti atakachokwenda kukaa uwanjani

Dar es Salaam. Siku 12 kabla ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga kucheza kwenye Uwanja wa Taifa, Bodi ya Ligi imetangaza tiketi za mchezo huo zitauzwa kulingana na namba za viti vya uwanja huo.

Mechi ya Simba dhidi ya Yanga unaotarajiwa kupigwa Septemba 30 ikiwa ni mechi yao ya kwanza msimu huu.

Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema kuelekea katika mchezo huo wameamua tiketi zianze kuuzwa mapema ili kila mmoja apate yake kwa muda sahihi.

"Tumeongea na Selcom kwamba tiketi ziuzwe kuendana na namba za viti (kuanzia tarehe 20) na kila mlango utumike katika kuingiza mashabiki uwanjani, tunahakikisha kila kitu kitaenda sawa katika mchezo huo," alisema Wambura.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya michezo kutoka Azam Tv, Baruani Muhuza, aliwasihi wateja wa ving'amuzi vyao kulipia ving'amuzi, lakini wasiache kwenda uwanjani.

"Tumehakikisha tutarusha matangazo haya kwa uzuri kabisa na kila mmoja aweze kupata kitu kizuri akiwa katika televisheni yake, lakini wasiache kwenda uwanjani hasa mashabiki ambao wanataka kuona timu zao uwanjani," alisema Muhuza.

Wakati huo huo: Afisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema anaamini katika mchezo huo watatoka na ushindi huku akiwasisitiza mashabiki wake wafike uwanjani kwa wingi.

Naye Afisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alitamba kuendeleza ubabe katika mchezo huku akiwabeza Simba kwamba wao ndio mabingwa wa kihistoria nchini.