Stars njia ya kupenya Afcon iko hivi

Thursday November 19 2020
stars pic

MATUMAINI ya timu ya taifa, Taifa Stars kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), yameonekana bado ni mlima mrefu baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na sasa itapaswa kushinda mechi zao mbili mwakani ili kutinga fainali hizo za Cameroon.

Stars ilipata sare hiyo nyumbani juzi usiku na kuifanya ifikishe alama nne na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Guinea ya Ikweta waliopo juu yao na vinara Tunisia walio na pointi 10 kila nchi ikicheza mechi nne mpaka sasa katika Kundi J.

Katika mchezo wa juzi bao la dakika 47 lililofungwa na mtokea benchini, Feisal Salum ‘Fei Toto’, liliipa Stars kupata sare hiyo nyumbani ikiwa ni siku chache tangu ilipotunguliwa 1-0 ugenini na Watunisia waliotangulia usiku wa juzi kwa bao la dakika 11 lililofungwa na Saif-Eddine Khaoui.

Ili Tanzania iende kwa mara ya pili mfululizo kwenye fainali hizo za Afrika ni lazima ishinde mechi mbili zilizosalia ikiwamo ya ugenini dhidi ya Equitorial Guinea na ile ya nyumbani watakayoikaribisha Libya wanaoshika mkia kwa sasa kundini hapo ikiwa na alama tatu kibindoni.

Stars ikishinda mechi hizo itafikisha alama 10 na kujihakikishia nafasi mojawapo ya kwenda katika fainali hizo, lakini kutoka sare ama kupoteza mbele ya wapinzani wao hao itajikwamisha.

Kwenye mechi ya juzi Stars ilipoteana kwenye kipindi cha kwanza kabla ya Kocha Etienne Ndayiragije kufanya mabadiliko ya kumtoa Himid Mao na kumuingiza Fei Toto aliyeleta uhai kwa kuituliza timu na kumpa unafuu Jonas Mkude kwenye eneo la katikati.

Advertisement

Hata hivyo, Tunisia walionyesha kudhamiria kuondoka na ushindi na kukata tiketi moja kwa moja kwa kutawala sehemu kubwa ya mchezo na kufanya mashambulizi mengi ambayo hata hivyo waliokolewa na mabeki wa Stars sambamba kipa wao Aishi Manula.

Mabadiliko mengine ambayo hayakuonekana kuwa na tija kwa Stars walipotelewa, John Bocco, Saimon Msuva na Farid Mussa na kuingia Adam Adam, Idd Selemani na Said Ndemla ambao walishindwa kupenya mbele ya Waarabu hao.

Katika kipindi cha kwanza Stars hawakutengeneza nafasi za kufunga na walikuwa wakipoteza mipira mingi lakini hata kipindi cha pili hawakuwa na mashambulizi mengi ya kutisha jambo ambalo timu yenye kuhitaji ushindi haiwezi kuwa na sifa kama hizo.


WASIKIE HAWA

Kocha Mohammed ‘Adolph’ Rishard, alisema Tanzania ina nafasi ya kufuzu fainali za Afcon kwa sharti la wachezaji kuongeza ari ya ushindani na kujiamini.

“Nimetazama mechi ya marudiano na Tunisia ilikuwa wazi kushinda baada ya kupigwa bao 1-0, hii sare imetupa ugumu zaidi, tukiongeza bidii ya kupambana, tunaweza kutimiza ndoto zetu,” alisema nyota huyo wa zamani Stars.

“Utamu wa mpira upo safu ya ushambuliaji na kipa, nje na hapo inakuwa shida, hili ni janga la taifa kwani hata kwenye klabu ambazo zinaonekana ni kioo kwa ligi kuu, wanaoongoza kwa ufungaji ni wageni, ndio maana nasema waongeze kujiamini,” alisema.

Beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa alisema Taifa Stars bado ina nafasi kubwa ya kufuzu michuano hiyo.

_____________________________________________

THOBIAS SEBASTIAN NA OLIPA ASSA
 

Advertisement