Simba yapata Wawa mpya

Saturday June 25 2022
Wawa PIC

Yussif Mubarik anayekipiga Asante Kotoko.

By Khatimu Naheka

SIMBA Juni 23, 2022 ilikuwa ikimalizana na Mtibwa Sugar katika mechi za kukamilishia ratiba ya Ligi Kuu Bara, huku mabosi wake wakiendelea kupiga hesabu za kimya kimya kumalizana na vifaa vyao tayari kwa kurudisha hadhi ya kikosi chao kwa msimu ujao wa mashindano.

Katika moja ya sajili ambazo Simba inaendelea kukamilisha ni kusaka mrithi wa beki Pascal Wawa ambaye aliagwa na mabosi hao walijifungia na mabeki wawili wa kazi nchini Ghana ili kushusha mmoja kwa ajili ya kusaidiana kazi na Enock Inonga na Mkenya Joash Onyango ambaye juzi alisaini mkataba wa kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo.

Mabeki ambao Simba imefanya mazungumzo nao ni pamoja na Yussif Mubarik anayekipiga Asante Kotoko anayesifika kwa ubora katika Ligi Kuu ya Ghana, pia yumo Vincent Atinga anayeichezea Madeama, iliyowahi kuvaana na Yanga katika makundi ya Kombe la Shirikisho 2016.

Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kutoka ndani ya Simba kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’, alikuwa Ghana kumaliza usajili wa kiungo mshambuliaji Augustin Okrah aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili.

Baada ya kumaliza dili hilo la Okrah alianza msako wa beki wa kati na kufanya mazungumzo na Mubarik aliyewahi kupigiwa hesabu na Yanga, ikiwa ni msako wa kusajili beki wa kati kabla ya kusitisha mipango hiyo baada ya kuona bado alikuwa na mkataba na klabu yake kipindi hicho.

Beki huyo mrefu na anayejua kuanzisha mashambulizi, majuzi alifanya mazungumzo na kigogo huyo wa Simba na alipotoka tu akamfuata Atinga anayepigiwa hesabu kutokana na kutajwa kuwa beki bora wa ligi ya nchini humo msimu uliomalizika.

Advertisement

Atinga yumo katika kikosi B cha timu ya taifa ya Ghana katika skauti ya taifa hilo kusaka wachezaji sahihi wa kuingia timu kubwa ya taifa na kama mipango itaenda sawa basi mmoja kati yake na Mubarik atakuja nchini kukipiga Msimbazi iliyoachana na Wawa aliyeagwa usiku wa jana mbele ya Mtibwa.

Tayari Try Again amesharejea nchini, lakini mapema Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alikaririwa kwamba usajili kwa upande wao unaendelea, japo bado hawajaamua kuuweka wazi zaidi ya ule ya Moses Phiri na kwamba unazidi kunoga na utawasapraizi mashabiki wa klabu hiyo.

Juu ya kocha mpya, Barbara alinukuliwa akisema mambo yamekamilika kwa kupatikana mmoja kutoka kwenye mchujo wa zaidi ya makocha 100 na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa ili kuanza maandalizi ya msimu mpya, akifichua kambi itakuwa nje ya nchi, lakini wala sio Afrika Kusini.

Simba ina nafasi ya kuongeza majembe ya kigeni kutokana na kuachana na Bernard Morrison aliyedaiwa kusaini Yanga, Rally Bwalya aliyeuzwa AmaZulu ya Afrika Kusini na sasa Wawa aliyemaliza mkataba.

Advertisement