Simba yaanza kiungo fundi

KIKOSI cha Simba tayari kipo Bukoba kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba, huku Kamati yake ya Usajili, chini ya Mwenyekiti wake, Kassim Dewji imeanza kufanyia kazi mapendekezo ya kocha wao Pablo Franco.
Inaelezwa kati ya mambo ambayo kocha huyo kutoka Hispania aliyataka uongozi kutekeleza ni kuwasainisha mikataba mipya nyota wote wa kikosi cha kwanza, kisha kuleta majembe mapya.
Katika utekelezaji huo, mabosi wa Simba wameanza mazungumzo ya kina na kiungo wao fundi, Hassan Dilunga ‘HD’ ili kumuongezea mkataba mpya, kabla ya kufuata wengine wenye mikataba iliyo ukingoni kisha waanze hesabu ya majembe mapya kuimarisha kikosi katika dirisha dogo.
Mwanaspoti limepenyezewa jana kuwa, Dilunga aliitwaa kwenye ofisi ya kigogo mmoja wa Simba, ili kujadili mkataba mpya kabla ya kuungana na wenzake kwenye safari ya mkoani Kagera.
Dilunga alikutana na kigogo huyo mwenye uamuzi ndani ya Simba na kuelezwa wapo tayari kumuongeza mkataba mpya baada ya ule wa awali wa miaka miwili wenye thamani ya zaidi ya Sh70 milioni unaoelekea ukingoni.
Baada ya kuelezwa hivyo Dilunga, aliomba muda wa kutafakari akienda pia kuzungumza na watu wake wa karibu kisha baadaye atoe uamuzi wa mkataba huo ambao angependa uongezwe thamani yake tofauti na unaomalizika.
“Mazungumzo ya pamoja yameanza ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Kocha Pablo, tunaamini kila kitu kitaenda sawa,” kilisema chanzo kilichoomba kuhifadhiwa jina lake, huku akibainisha mkataba wa HD umesaliwa na miezi mitano ndio maana wameanza naye kwanza.
Kwa mujibu wa sheria za usajili zinazotambulika ni kwamba klabu yoyote inaruhusiwa kufanya mazungumzo na hata kumpa mkataba wa awali akiwa na mkataba usiozidi miezi sita, ila kwa klabu yake pia kufahamishwa na kuridhia.
Dilunga alipotafutwa na simu kuulizwa juu ya jambo hilo, alisema; “Mkataba nilionao bado haujaisha, tusubiri kwanza mwisho wa msimu kila kitu kitakuwa wazi kama nitaongeza mpya au vinginevyo.”
Kwa vipindi tofauti, Dilunga aliwahi kuhusishwa na klabu yake ya zamani Yanga, lakini mara zote Simba ilifanikiwa kuzima dili hilo kwa kumbakisha Msimbazi na hivi karibuni aliivusha timu yake makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufunga bao la kufutia machozi wakati Simba ikilala 2-1 mbele ya Red Arrows ya Zambia.
Mbali na Dilunga wachazeji wanne wa kigeni akiwamo Joash Onyango, Pascal Wawa, Chriss Mugalu na Rally Bwalya nao mikataba yao ipo mwishoni, lakini tayari Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ mara baada ya mechi hiyo ya ugenini dhidi ya Red Arrows alisema wanakwenda kufanya marekebisho kwa ajili ya kusajili wachezaji wanaoweza kwenda kupambana.
“Tunafanya marekebisho na kuboresha timu kwa ajili ya kuchukua kombe la Shirikisho Afrika,” alikaririwa Try Again.
Ofisa Mtendaji wa Simba, Barbara Gonzalez alisema watafanya uamuzi mgumu.