Simba jeuri, yashtua Angola

Simba jeuri, yashtua Angola

SIMBA chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez wamekumbuka yaliyowakuta Namungo nchini Angola, wakawapigia simu Red Arrows ya Zambia fasta halafu wakajiongeza na sasa mipango yao imewashtua Clube de Agosto wanaocheza nao Jumapili jijini Luanda.

Arrows walitolewa na Waangola hao hivikaribuni baada ya kufungwa nyumbani bao 1-0 na ugenini kulazimisha sare ya bao 1-1. Lakini mmoja wa viongozi wa Simba ameweka wazi kwamba baada ya Arrows kuwapa fitna za wenyeji wameamua kukodi ndege ambayo itawasubiri jambo ambalo limewashtua De Agosto na wameanza mipango mizito ikiwemo kuita mashabiki kwa wingi.

Tofauti na mechi nyingine zote za miaka ya hivikaribuni, Simba wameamua kwamba watakaa Angola saa 48 tu. Tathmini ya kishushu ambayo Simba wameifanya wamegundua kuwa Angola kuna changamoto kubwa ya usafiri wa anga kutokana na uchache wa ndege zinazotua humo kutokea nje jambo ambalo limewafanya waamue kutumia ndege ya kukodi kwa safari ya kwenda na kurudi nchini humo.

Simba wanaamini kuwa iwapo watatumia usafiri wa ndege za kawaida ama wangepata changamoto za kuchelewa kufika au kuondoka huko na suala ambalo lingepelekea kuathiri maandalizi yao ya mechi ya marudiano.

Lakini mbali na kwenda na kurudi Angola kwa ndege ya kukodi, Simba imepanga kutua nchini humo siku moja kabla ya mechi, kwa maana ya Jumamosi asubuhi na jioni itafanya mazoezi katika Uwanja wa 11 de Novembro uliopo jijini Luanda ambao utatumika kwa mechi hiyo kesho yake, Jumapili, Oktoba 9 na baada tu ya mchezo huo, msafara wa Simba utapanda ndege kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi itakayofuata.

Sababu kubwa iliyoufanya uongozi wa Simba kwa kushauriana na benchi la ufundi chini ya kocha Juma Mgunda kuamua timu hiyo isikae Angola kwa muda mrefu ni kuepuka hujuma za wenyeji ambazo ziawafanya wachezaji kuathirika kisaikolojia.

“Wamekuwa na tabia ya kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu pinzani pindi wanapokuwa nchini mwao kwa kutumia mbinu mbalimbali hivyo ukikaa muda mrefu kule, ni rahisi kwa wachezaji kujawa hofu. Hii kwenda kwa muda mfupi ina faida maana wachezaji wataamkia siku ya mchezo hivyo hawatokumbana na mambo mengi ya nje ya uwanja,”alidokeza kigogo mmoja wa Simba huku akiongeza kuwa tayari mashushushu wao wapo Angola.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alikiri kwamba; “Kikosi kitaondoka kwenda Angola siku ya Jumamosi, Oktoba 8 na siku ya Jumapili ndio ya mchezo na baada tu ya mechi tutaondoka kurejea Dar es Salaam siku hiyohiyo. Maandalizi kwa ajili ya safari hiyo yamekamilika kwa asilimia kubwa.”

Simba imekuwa na rekodi nzuri kimataifa kwenye misimu ya hivikaribuni ingawa changamoto kubwa imekuwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Rekodi za Simba ndizo zimeiongezea Tanzania Bara alama na kuingiza timu nne kimataifa msimu huu.