Sharks waitolea macho Ligi Kuu

Sharks waitolea macho Ligi Kuu

YANAYOJIRI ndani ya klabu ya Kariobangi Sharks yana umuhimu kwa Wazito FC na Vihiga Bullets zinazopambana kuepuka kushuka darajani.

Tayari Mathare United imeshashushwa Ligi Kuu Kenya huku sasa ikisubiriwa timu moja kuungana nao na nyingine itakayomaliza nafasi ya 16 kucheza hatua ya ‘playoff’ na timu itakayomaliza nafasi ya tatu National Super League.

Kamati ya Mpito Shirikisho la Soka Kenya (FKF) iliyoteuliwa na Waziri Balozi Amina Mohammed saa chache tu baada ya Kamati Shikilizi ya FKF kumaliza muda wake wa miezi sita iliishushia rungu nzito Mathare United.

Kilichopelekea Mathare United ambao wamedumu kwenye ligi kwa zaidi ya miaka 20 kushushwa daraja inatokana na wao kushindwa kutokea uwanjani kwa mechi tatu mfululizo dhidi ya Bandari FC, Ulinzi Stars na Sofapaka.

Macho sasa yameelekezwa kwa Kariobangi Sharks hususan baada ya wiki iliyopita kutoa taarifa kwa mashibiki wao kuwa timu haitocheza mchezo wa ugenini dhidi ya AFC Leopards na kwamba watawatarifu endapo au wakati ligi itarudi.

Mechi mbili zinazofuata za Kariobangi Sharks ni dhidi ya Bandari FC na Talanta FC na kama watasusia kuingiza timu uwanjani pasipo na sababu ya kuiridhisha kamati ya mpito FKF, basi nao pia watashushwa.

Endapo hilo litatokea, timu mbili ambazo zinapaswa kushushwa daraja zitakuwa zimeshafahamika nazo ni Sharks na Mathare United hivyo kuipa ahueni Vihiga Bullets, Wazito FC na Nzoia Sugar ambazo hazipo salama.

Mathare United ambao kabla ya kushushwa daraja walikuwa wa mwisho kwenye msimamo wameirundikia lawama iliyokuwa kamati shikilizi FKF kwa kushindwa kuwalipa mgao wao kwa muda unaotakiwa hali iliyowachangia kushindwa kupeleka timu uwanjani kwa mechi tatu mfululizo. Mwenyekiti wa Mathare United, Bob Munro alimuandikia mkuu wa secretariat ya kamati ya mpito FKF, Lindah Oguttu, akihoji kama mamlaka hiyo ilikua na nguvu za kisheria kuwashusua Ligi Kuu.

“Baada ya kushiriki tangu 1999 Ligi Kuu Kenya kwa misimu 24 mfululizo, je ni sahihi na haki na pia kisheria kwa kamati ya mpito kuisimamisha na kuishusha MUFC au klabu yoyote kwasababu mtangulizi wake kamati ya shilikilizi ambao wewe ulihudumu kama mkuu wa secretariat mara kadhaa kushindwa kulipa mgao wa kila mwezi kwa wakati?” ilihoji barua ya Munro.