Serengeti Boys wapewa neno

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza Tanzania watakuwa wenyeji wa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe  amewataka vijana wa Serengeti Boys kuyashika wanayofundishwa ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019) kwa vijana chini ya miaka 17,mwakani.
Dk. Mwakyembe ameyasema hayo alipowatembele kambini vijana hao asubuhi ya leo wakati wa mazoezi kwenye Uwanja wa Karume jijini hapa.
"Taifa linaelewa kuwa mwakami, tutakuwa uwenyeji  wa mashindano makubwa, nyie ndiyo mabalozi wa Watanzania wote katika mashindano nayo.
" Ninauhakika kuwa mtaifanya bendera ya Tanzania ipepee kimataifa, Serikali yote ipo pamoja nanyi, zingatieni sana mfundishwayo," alisema waziri huyo.
Naye nahodha wa Serengeti Boys, Morris Michael 'Chuji' amefurahishwa na ujio huo wa waziri na kusema watalipigania taifa kwa nguvu zao zote.
"Tunamshukuru waziri kwa kutupa hamasa ya kuendelea kujiandaa na mashindano, jukumu lililopo mbele yetu ni zito ila tutajitahidi kuyashika yote ambayo tunafundishwa ili tufanye vizuri" alisema nahodha huyo.
Mbali na uwenyeji wa Tanzania katika mashindano hayo ya vijana Afrika pia mwishoni mwa mwaka huu itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Cecafa kwa vijana.