Rage: Mkude jitambue sasa

SIKU moja baada ya Kiungo wa Simba na Taifa Stars, Jonas Mkude kuomba radhi kupitia mitandao ya kijamii, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo Ismail Rage amemtaka kujitambua.

Uongozi wa Simba ulitangaza kumsimamisha Mkude hivi karibuni kwa madai ya utovu wa nidhamu huku akikosa mechi muhimu dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe ambao Simba iliwaondosha katika mashindano ya klabu bingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti Rage, alisema licha ya Mkude kuomba radhi juzi, alichelewa kwani kama alitambua kosa lake angekiri siku hiyo hiyo huku akiwataka viongozi kumrejesha kundini na aenndelee na majukumu yake.

“Amejua na kujutia alichokifanya mpaka viongozi wakamuweka kando na wenzake, wanasimba wasimbeze kafanya uugwana sana, na hata viongozi wamsamehe kwa ujasili aliouonyesha,”

“Nikiwa Mwenyekiti wa Simba nilimsimamisha marehemu Mafisango kwa utovu wa nidhamu na yeye alijifikiria na kuomba radhi, nikaona ni vyema kumsamehe baada ya kuonyesha kujutia na kuumizwa na kile alichokifanya hivyo kama kiongozi na mzazi pia niliona ni busara kumsamehe na aliporejea uwanjani alifanya maajabu,”alisema Rage.