PWANI WAIPIGIA MAGOTI SERIKALI KURUDISHA MICHEZO

MASHABIKI wa michezo katika kaunti ya Kilifi wanaipigia magoti serikali ya kaunti hiyo kuruhusu vijana kuendelea na kuendeleza michezo katika viwanja mbali mbali katika kaunti hiyo.

Wanasema kuendelea kuifungia michezo katika eneo hilo kutaweza kuongeza visa vya mimba za utotoni kwa vijana wa kike na kufanya idadi kubwa kujiingiza kwenye magenge ya utumizi wa madawa ya kulevya na utovu wa maadili katika jamii.

Akizungumza na Mwanaspoti mwenyekiti wa marefa katika eneo la Rabai kaunti ya Kilifi Said Mkamba Dzaya kwa jina maarufu “chii chone” anasema kwamba vijana katika eneo hilo wameathirika pakubwa kutokana na kufungiwa kwa michezo kwa sababu ya msambao wa virusi vya janga la Covid-19 nchini.

Said anasema kuwa mbali na kuathirika kwa vijana pia kumefanya viwango vya michezo mbali mbali ikiwemo soka kushuka katika kaunti hiyo.

Amezidi kusema kwamba baada ya corona kuchipuka nchini vijana wengi wa eneo hilo wamekua wa kihangaika wasijue cha kufanya huku wengi wakipotelea kwenye uraibu wa pombe.

Said amezidi kusema kwamba kutokana na hilo mimba za mapema zimeshuhudiwa na vijana wa kiume wakijitosa kwenye magenge ya utumizi wa mihadarati.

Kutokana na hilo wadau mashabiki na wajereketwa wa michezo katika kaunti hiyo ya Kilifi wangependa michezo iweze kuruhusiwa kurudia hali yake ili waweze kuwanusuru vijana ambao kuna hatari ya kuangamia kwa madawa ya kulevya.

“Tunaiomba serikali ya kaunti ya Kilifi iweze kuruhusu michezo iendelee kwani vijana wanapotoka mitaani kutokana na kukaa bure bila kufanya chochote huku wale wa kike wakipata mimba kwa sababu ya ukosefu wa kujihusisha na michezo mitaani,” asema.

Aidha Mkamba ameiomba idara ya utawala katika eneo hilo kuweka mikakati kabambe kuona kuwa wanaruhusu michezo kuendelea kwa vilabu kufuata utaratibu unaotakiwa na wizara ya afya na serikali.

Aliongeza kusema kusalia nyumbani kwa vijana bila kujishugulisha na chochote mitaani kumeleta athari kubwa na uvunjifu wa maadili kwa jamii katika kaunti hiyo.

Anasema kutokana na tamko la rais kuwa sasa mkusanyiko wa idadi ya watu unao ruhusiwa ni hadi wato 100 basi machifu na manaibu wao wanatakiwa kujipanga kikamilifu kuona kuwa timu mbali mbali za kaunti hiyo zinarudia shuguli zake za kawaida kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya nchi.

“Tunatoa rai kwa machifu na manaibu wao katika eneo letu waweke mikakati kuona kuwa vijana wetu wanarudi viwanjani kama tunavyoona katika kaunti zingine nchini, kwani kuzidi kuwabana ndio kunapelekea kuongezeka kwa visa vya utovu wa nidhamu mashinani, kikubwa michezo irudi ili vijana wawe bize na michezo kama ilivyokuwa hapo awali.”