Pamba yarejea Ligi Kuu Bara baada ya miaka 22

Muktasari:

  • Katika mchezo wa leo kikosi ambacho kimeweka historia ya kuirejesha kwenye Ligi Kuu Pamba kwa maana nyota ambao walianza kulikuwa na Shaban Kado, Frank Kavinea, Hassan Mwasapili, Salehe Seif, John Ntobesya, Daniel Joram, Mudathir Said, Michael Samamba, Salum Kipemba, Issa Ngoah na Ismael Ally.

TP Lindanda wana Kawekamo timu ya Pamba Jiji FC imerejea tena Ligi Kuu Bara na kuwakata kiu mashabiki wa soka wa Jiji la Mwanza ambao wamesubiri kwa zaidi ya miaka 20, huku kocha Mbwana Makatta akiandika historia ya kuzipandisha daraja timu nne ndani ya misimu saba.

Mabingwa hao wa Ligi ya Muungano mwaka 1990 wamerejea tena baada ya kuitandika mabao 3-1 Mbuni FC katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Championship ambao umepigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

Ushindi huo imeifanya timu hiyo kufikisha alama 67 katika nafasi ya pili ikizidiwa alama tatu na bingwa mpya wa Champioship 2023/24, Ken Gold FC, yenye pointi 70 wakati ambapo Mbeya Kwanza na Biashara United Mara zitatafuta nafasi ya kupanda kupitia mtoano (playoff). Mshindi kati yao atakutana na mshindi wa play-off ya Ligi Kuu Bara itakayozikutanisha timu ya 13 na 14.

Katika mchezo wa leo kikosi ambacho kimeweka historia ya kuirejesha kwenye Ligi Kuu Pamba kwa maana nyota ambao walianza kulikuwa na Shaban Kado, Frank Kavinea, Hassan Mwasapili, Salehe Seif, John Ntobesya, Daniel Joram, Mudathir Said, Michael Samamba, Salum Kipemba, Issa Ngoah na Ismael Ally.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilianza kwa kasi huku TP Lindanda ambayo ilikuwa inahitaji sare au ushindi ikiwa na presha kubwa ya kutaka kupata bao la mapema na kumaliza kazi.

Huku wakipata sapoti kubwa kutoka kwa zaidi ya mashabiki 1,000 kutoka jijini Mwanza wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Meya wa Jiji la Mwanza, Biku Kotecha, Mkuu wa Wilaya Magu, Joshua Nasari, Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi, Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano na pia mashabiki wa timu hiyo waishio hapa hapa jijini Arusha.

Iliichukua Pamba Jiji FC dakika mbili pekee kuandika bao la uongozi kupitia Kwa Salum Kipemba kwa mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa Mbuni FC, Paul Bukaba kunawa ndani ya boksi, bao ambalo lilidumu kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Pamba ilirejea kwa kasi na kupeleka presha ya hatari langoni kwa Mbuni FC iliyozaa bao la pili katika dakika ya 48 kupitia Mudathir Said akiunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Daniel Joram.

Bao hilo liliifanya Mbuni FC kuanza kulisakama lango la Pamba FC kama nyuki huku wakisahau kulinda lango lao na kumpa mwanya Mudathir Said katika dakika 63 kuwanyanyua tena mashabiki wa Pamba ambao walifurika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kupeleka rasmi furaha Mwanza kwa kuandika bao la tatu.

Mbuni FC ilijipapatua na kuandika bao la kufutia machozi katika dakika ya 90 kupitia Naku James kwa mkwaju wa penalti.

Pamba imemaliza msimu wa 2023/24 wa Championship kwa kucheza mechi zote 30, ikishinda 20 sare saba na kupoteza tatu huku ikifunga mabao 54 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 18 pekee.

TP Lindanda kurejea Ligi Kuu inamfanya kocha wa timu hiyo Mbwana Makata kuweka rekodi ya kuwa kocha pekee Tanzania ambaye amezipandisha daraja timu nne ndani ya misimu saba.

Alianza na Alliance FC msimu wa 2017/18, Polisi Tanzania FC 2018/19, Dodoma Jiji FC 2019/20 na Pamba Jiji FC 2023/24 huku akitafuna mfupa mgumu ambao uliwashinda makocha wengi kwa zaidi ya miaka 20 kuipandisha Pamba.