Pablo: Kuna sapraizi inakuja Mwanza

KOCHA wa Simba, Pablo Franco amesema mara nyingi mechi za dabi wanayocheza suala la rekodi linakuwa halina nafasi, mambo mengi huwa ni sapraizi ya hapo kwa hapo lakini wanajiandaa kupata ushindi.
Pablo alisema matokeo yao ya hivi karibuni tangu walivyocheza na Yanga si mazuri hasa kwenye ligi lakini mechi kubwa kama hiyo huwa inaamuliwa na mambo ya kiufundi zaidi.
Alisema mechi ya awamu hii lazima mshindi apatikane hata kwenye hatua ya mikwaju ya penalti na hilo kwao wanalifanyia kazi ili kuona kama litatokea waweze kufanya vizuri tofauti na ilivyokuwa michezo ya nyuma.
“Kama ambavyo wenzetu walitenga muda wa kutufuatilia na kuja kuangalia mechi zetu nasi tumefanya jambo kama hilo ili kuona namna gani tunacheza mechi hiyo kwa ubora dhidi yao ili kupata ushindi,” alisema Pablo na kuongeza:
“Mechi iliyopita dhidi ya Yanga na nyingine zilizofuata maandalizi na mbinu tutakazotumia kwenye mechi hiyo itakuwa tofauti kabisa ili kuona tunakuwa bora zaidi ya mpinzani.
“Katika mazoezi yetu ya wakati huu tunafanya yale tuliyokuwa na mapungufu nayo ili kuwa bora pamoja na namna gani tutakwenda kuwazuia wapinzani kutokana na uimara wao na namna gani tutakwenda kuwashambulia kutokana na mapungufu yao.
“Wachezaji wangu huu mechi ipo mikononi mwao wao wana kila sababu ya kupambana na kuhakikisha Simba inafikia malengo yake ya kupata ushindi na kusonga kwenye hatua inayofuata. Tupo karibu na kutetea taji hili wachezaji mbali ya mazoezi huwa nazungumza nao mmoja kwa mmoja.”