Olunga anafukuzia cheki nzito Qatar

NAHODHA wa Harambee Stars, Michael Olunga anafukuzia cheki nzito ya dola 100,000 (Sh11.5 millioni) baada ya kuteuliwa kuwania tuzo la mchezaji bora wa msimu 2021/22.

 Mbali na Olunga, yupo mchezaji mwingine Mkenya mzaliwa wa Mombasa Hashim Ali aliyeteuliwa vile vile kuwania tuzo hilo. Ali amekuwa kwenye fomu ya kutisha akiichezea klabu ya Al Rayyan.

Olunga amekuwa moto wa kutisha toka alipojiunga na Ligi Kuu ya Qatar mwaka jana inayoendeshwa na Shirikisho la soka la Qatar (QFA).

Hata hivyo straika huyo wa Al Duhail atakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa mastraika Akram Afif wa Al Sadd na raia wa Angola, Jacinto Dala anayeichezea Al-Wakrah.

Tayari Olunga amekwachua tuzo la kiatu cha dhahabu Mansour Moftah Award baada ya kumaliza msimu kwa kupachika mabao 24, akimpiku mpinzani wake wa karibu nahodha wa Ghana Andre Ayew kwa magoli tisa.

Kiungo wa zamani wa Arsenal, Santi Carzola naye alijumulishwa kwenye listi kabla ya jina lake kuondolewa na pengo kujazwa na Dala. Dala amepachika magoli 11 ikilinganishwa na sita za Carzola kwenye Ligi Kuu ya Qatar Stars League (QSL) iliyofika kikomo hivi majuzi.

Kocha Mreno Luis Castro aliyemnoa Olunga kabla yake kutimuliwa katikati ya mwezi Machi mwaka huu, naye anawania tuzo la kocha bora wa msimu.

Tuzo la mchezaji bora wa msimu QFA liliasisiwa 2006 sambamba na tuzo la kocha bora wa msimu na kila anayeibuka mshindi hulambishwa donge nono la dola 100,000.