Nabi: Uchawi wangu ni huu hapa...

YANGA wanatamba watakavyo kwa sasa mtaani kutokana na ubora wao na sasa jeuri inazidi wakisema timu yao ni kama iwe inacheza kila siku tu kwa kuwa wana uhakika wa kushinda nyingi, lakini kocha wao Nesreddine Nabi amefichua kitu juu ya ubora wa timu yake.

Nabi ameiongoza Yanga kwenye mechi sita za mashindano na zote akishinda akianza na Ngao ya Jamii alipoibutua Simba kwa bao 1-0, kisha kushinda michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara, huku chama lake likipiga soka la kusisimua la pasi nyingi na kuwapagawisha mashabiki.

Hata hivyo, kocha huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa kupanda kwa ubora wa timu yake kuna mambo mawili makubwa ambapo siri ya kwanza ni kocha msaidizi wake, Helmy Gueldish ambaye sasa ameanza kuonyesha ubora wa kazi yake.

Nabi alisema Gueldish ambaye ni kocha wa mazoezi ya viungo alijua kwamba baada ya miezi michache ataanza kuonyesha ubora wake katika kuwapa ubora wachezaji wake na kwamba baada ya muda makali zaidi ya timu hiyo yataongezeka.

Kocha huyo alisema haikuwa kazi rahisi kumuondoa Gueldish ambaye ana elimu ya shahada ya uzamili ya mazoezi hayo aachane na klabu kubwa ya Tunisia ya Etoile du Sahel kisha aje Jangwani.

Yanga ilipoanza kwa kushinda bao 1-0 katika mechi zake tatu mfululizo ikiwamo ya Ngao ya Jamii kuna mashabiki walikuwa wakiibeza wakidai inakata pumzi dakika 45, lakini mechi zilizofuata imeshinda mabao 2-0 dhidi ya KMC, Azam na juzi ikaifumua Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 ikitoka nyuma.

“Nilikuwa namwambia kila kitu kwamba mashabiki wanalalamika kwamba eti timu inapungua pumzi akawa anakasirika alijua kwamba muda ambao aliniambia wachezaji watakuwa tayari ulikuwa haujafika na wala Yanga haikuwa inakata pumzi,” alisema Nabi.

“Huyu ni kocha bora ambaye anajua kutengeneza ufiti wa wachezaji na anaijua kazi yake kuliko watu walivyodhani na sasa kazi yetu kama makocha inakuwa fupi kuingiza mbinu kitu ambacho sasa kinakamilisha kazi yetu hapa.”

Nabi aliongeza mbali na ubora wa Gueldish katika mazoezi ya viungo pia jamaa anajua kuchambua ubora wa wapinzani kazi ambayo huwa anaifanya taratibu siku mbili kabla ya mchezo wowote.

Kocha huyo alisema kuwa juu yote anamshukuru bilionea wa klabu hiyo, Gharib Mohamed ambaye amekuwa akitaka kuona Yanga inasimama imara akisema alimpa karibu kila kitu kuhakikisha wanapata wachezaji bora.

“Nafahamu soka la Afrika kuna wakati watu wenye fedha kama Gharib huwa wanataka kuwaona wachezaji wao wanasajiliwa, lakini Gharib hayupo hivyo alinisikiliza mimi kama kocha niseme namtaka mchezaji gani na karibu wote tuliowataka niliwapata na sasa timu inafurahia matunda ya kazi nzuri,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tuna kikosi kilichounganishwa na wachezaji bora ambao tuliwasajili tulifanya kazi nzuri ya kushirikishana ndio maana nilichelewa hata kwenda kupumzika baada ya ligi iliyopita ili tupate wachezaji sahihi ambao watatupa thamani tukishirikiana na Hersi (Injinia Said).”