Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwashuiya na mkewe mapenzi ni motomoto

Muktasari:

  • Yasahau yale mabao yake ya umbali mrefu na pasi za mwisho anazopiga pale Taifa na Uhuru akiwa ndani ya jezi ya Yanga. Hebu potezea pia kasi yake uwanjani na mambo mengine ambayo unavutiwa nayo kwake akiwa uwanjani.

ACHANA kwanza na kasi yake pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yakaushie yale mashuti yake ya kipindi kile kabla hajaanza kusumbuliwa na maumivu ya goti.

Yasahau yale mabao yake ya umbali mrefu na pasi za mwisho anazopiga pale Taifa na Uhuru akiwa ndani ya jezi ya Yanga. Hebu potezea pia kasi yake uwanjani na mambo mengine ambayo unavutiwa nayo kwake akiwa uwanjani.

Unaambiwa Geofrey Mwashiuya akiwa nyumbani mapenzi ni moto. Yaani ule ufundi wake pale Taifa na mbwembwe zote ndani ya jezi ya Yanga huwa zinaishia mlangoni na akifika tu nyumbani ni mahaba mazito yeye na mkewe.

Kama ulikuwa hufahamu jamaa alishavuta jiko kitambo tu na hapa mjini wala haangaiki na wale vicheche ambao wakiwaona mwanaume wana ‘six packs’ na chenji kidogo tu, basi inakuwa tabu.

Sasa Mwanaspoti lilifunga safari na kutua kwa winga huyo aliyejiunga na Yanga akitokea Kemondo ya Mbeya miaka mitatu iliyopita na kuzungumza naye mambo kadhaa. Mwashiuya anaishi Mabibo jijini Dar es Salaam, eneo ambalo pia anaishi kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya. Pata simulizi ya hapo nyumbani kwake.

HAJUI KUPIKA

Unaweza kucheka lakini katika kitu ambacho kinampa tabu Mwashiuya ni kupika kwani hakuna chakula cha aina yoyote au mboga ambayo anaweza kupika. Yaani jamaa anajua tu kuwasha jiko lakini baada ya hapo labda apike uji ama chai, vingine mmh!

“Nilivyohamia hapa nilikuwa nakula juu kwa juu, lakini kuna muda nilikuwa naishi na mdogo wangu ambaye alikuwa mtaalumu wa kupika ndio alikuwa anafanya makeke lakini mimi siwezi kitu,” anasema Mwashuiya ambaye mkataba wake na Yanga unamalizika msimu huu.

“Unaweza kunikuta jikoni lakini kitu ambacho naweza kufanya ni kuchemsha chai ndio nahisi hicho naweza kufanya kwa ufasaha,” anafunguka.

MAJI, JUISI NDIO HABARI

Mwashuiya anasema kila anapokuwa nyumbani mkewe Zainabu lazima amtengenezee juisi ya mchanganyiko wa matunda ambayo anaweza kunywa hata lita mbili kwa siku baada ya kula akiwa amepumzika tu.

“Nakunywa sana juisi, naweza kufika hata lita mbili kwa siku lakini maji ndio nakunywa zaidi nikiwa hapa nyumbani au kambini, kwani nikifanya hivyo huwa na morali wa kufanya mazoezi zaidi,” anasema.

MENYU YAKE JE

“Napenda sana kula pilau, hasa hapa nyumbani, lakini hata kambini kama litakuwa linapatikana huwa nakula. Unajua kule muda mwingine tunabadilishiwa vyakula tofauti na nyumbani ninakula muda wote ninapotaka,” anasema.

“Mke wangu Zainabu analijua hilo maana haiwezi kuisha mwezi bila kulipika, hivyo nashukuru kupata mwanamke anayejua mume anapenda nini.

“Nikila chakula hicho najioni mwili wangu huwa sawa na furaha zaidi, kwani nakipenda tangu nikiwa mdogo. Mama yangu alikuwa ananipikia pilau sana, alifanya nisicheze mbali na nyumbani,” anasema.

KUMBE MTATA

Mwashiuya anasema kuna kipindi Yanga ilisafiri kwenda Zambia kucheza na Zanaco na katika safari hiyo alikuta viatu vyake vya mazoezi vimeibiwa na baadaye alimkuta navyo jamaa yake (anaficha jina), amevaa katika mazoezi ya kitaani kwake maeneo ya Kifa Kigogo.

“Nikiwa nyumbani napenda kufanya mazoezi kitaa, siku niliporudi kutoka katika majukumu ya klabu, nikamkuta jamaa yangu amevivaa mazoezini nikamwambia viatu hivyo ni vyangu akawa anabisha, basi nikamwambia nampeleka polisi.

“Alipoona mambo magumu akavivua na kunikabidhi, basi kila mtu akaendelea na yake na bado tunafanya wote mazoezi, lakini kwa watu wa pale mtaani kwangu wana ushirikiano mzuri na wananilindia vitu vyangu ninaposafiri,” anasema.

ANALEA

Winga huyo anaweka wazi maisha ya nyumbani ni mazuri zaidi kwa kuwa anapata muda wa kukaa na mtoto wake aliyemtambulisha kwa jila la (Babra) lakini kambini mara nyingi anakuwa na wenzake na wanazungumzia kazi zaidi.

“Kambini nipo kwa ajili ya kazi, lakini hiyo kazi ninafanya kwa ajili ya familia sasa ninapokuwa na familia yangu najisikia faraja hasa ninapokaa na mtoto wangu na mke wangu wanakatiza mbele yangu na hata muda mwingine kutaniana kidogo,” anasema.

Mwashuiya anasema anaishi na mke wake, anaelezea jinsi anavyofurahia maisha ya ndoa kwamba yanampa faraja ya kupambana.

“Tangu nimeanza kuisha na mke wangu , najiona nipo mazingira sahihi ,nafanyiwa vitu kwa wakati, kama muda wa kula, ratiba nyingine muhimu ikiwemo kwenda mazoezini, tofauti na kipindi nilichokuwa msela,” anasema.

“Yapo majukumu ambayo namsaidia mke wangu kama kufua na kufanya usafi nikiwa nyumbani, lakini muda mwingine huwa namsaidia malezi ya mtoto wetu ili aone mapenzi ya wazazi wote wawili,” anasema Mwashuiya.

MECHI YA SIMBA

Mwashuiya anasema pindi inapokaribia mechi ya Simba na Yanga anapokuwa nyumbani huwa anatumia muda mwingi kuifikiria mechi hiyo kwani ni rahisi kupata jina au kuonekana si mali kitu tena.

“Naitazama mechi ya watani wa jadi kwamba lazima mchezaji ajitambue kwa kuwa inawafanya kujulikana kwa jamii, kutokana na jinsi inavyowajaza mamilioni ya mashabiki ndio maana huwa natenga muda wa kutosha kuifikilia mechi hiyo,” anasema.