Morrison amng’oa Katibu Yanga SC, mwenyewe ajibu mapigo

Thursday November 19 2020
morison pic

KLABU ya Yanga imetangaza kumsimamisha Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama, Wakili Simon Patrick, huku ikielezwa sakata la winga Mghana, Bernard Morrison ni moja ya sababu iliyomchomoa kigogo huyo ambaye naye fasta ameamua kujibu mapigo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla imeeleza Wakili Simon amesimamishwa baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichoketi kwa dharura Novemba 17 kufikia uamuzi wa kumsimamisha kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali.

Kamati ya Utendaji pia imeeleza imeunda kamati maalum itakayochunguza na kumhoji Patrick kisha kitakachobainika kitawasilishwa kwa kamati hiyo.

Hata hivyo, mapema wiki iliyopita, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Athuman Kihamia aliibua madai mbalimbali ya mmoja wa watendaji huku akishindwa kumtaja jina.

Wakati Yanga ikitangaza uamuzi huo uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kwamba zipo tuhuma mbalimbali zinazomkabili Simon ambazo zitatakiwa kutolewa majibu.

Simon anakabiliwa na tuhuma za kushindwa kusimamia vyema sakata la Morrison katika mawasiliano na winga huyo, ambaye kwa sasa yupo Simba huku kukiwa na kesi nne zikiwa kwenye ofisi za TFF na nyingine ikipelekwa Mahakama ya Usuluhishi ya Kimichezo (CAS).

Advertisement

Pia ikielezwa amekuwa na ukaribu na viongozi wa juu wa Simba jambo ambalo limewafanya mabosi wenzake kuhisi kama anaihujumu timu, lakini mwenyewe (Simon), kupitia ukurasa wake wa Instagram (Simon.esq) alianika orodha ya vitu vitano anavyotuhumiwa nayo na kuvifafanua.


VIKAO VYA SIRI

Wakili Simon alithibitisha kuandika yeye kilichoonekana kwenye akaunti hiyo.

“Nakiri kukutana na Mtendaji mwenye rank kama yangu kama alivyotaja maeneo ya Yatch Club, lakini sio vikao vya siri, kwani kilichonikutanisha naye mtendaji huyo ni suala muhimu ambalo viongozi watatu walinituma na baada ya kikao hicho nilirejesha taarifa na hii naongelea ilikuwa tarehe 20/10/2020.”


ISHU YA SENZO

Juu ya tuhuma kwamba ana hofu ya kuporwa namba na Mshauri Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa, Wakili Simon aliandika;

“Mimi nakaimu nafasi ya katibu mkuu kwa muda lakini nimeajiriwa kama Mkurugenzi wa Sheria, hivyo basi siwezi kumuhofia Mr Senzo kwani yeye sio mwanasheria bali ni mshauri mkuu wa klabu, kukaimu nafasi maana yake ni unashikilia kwa muda viongozi wanaweza kupiga simu moja tu kwamba kuanzia leo sio kaimu tena na nikatii hofu sijui inatokea wapi.

Masuala mengine aliyoandika ni Kuhujumu kesi ya Morrison, kufuta kesi ya Morrison TFF na kutopokea simu za Mwenyekiti na kuandika kwamba kuna kesi nne kwenye ofisi za TFF na zote zimeweka kando kwa sasa, huku akifichua kuna kesi yao iliyopo CAS dhidi ya Morrison akisema kwa uzoefu wake anaamini kila kitu kitatiki.

Wakili alifichua kesi hiyo ya CAS ambayo baadhi ya mashabiki walidhani ni changa la macho, alisema imefunguliwa kwa namba CAS2020/A/7397 ikiwa ni maana ni kesi ya 7397 kwa vile mahakama hiyo ya Michezo ya Kimataifa inapokea kesi kutoka nchi wanachama wa FIFA.

Juu ya kesi zilizopo TFF ni ile ya Morrison kuhongwa Dola 5,000 ili kuihama Yanga, ishu ya mkataba wake Simba wenye upungufu na pingamizi la usajili wake na ile ya kipa ya Ramadhani Kabwili ya kudaiwa kuhongwa.

Alipoulizwa na Mwanaspoti jana kama kile kilichoandikwa kwenye akaunti ile ni chake, Wakili Simon alithibitisha aliyoyaandika ni yake.

“Kweli hiyo ni akaunti yangu na mimi ndio niliandika mwenyewe, alisema kwa kifupi.”

____________________________________________________

 By Khatimu Naheka, Imani Makongoro na Thomas Ng’itu

Advertisement