Mkenya anatua, Manula anatoka Simba

LICHA ya kwamba wanafanya siri kubwa, lakini kuna kila dalili Simba watapokea ofa ya Mamelody Sundowns kwa kipa wao, Aishi Manula.

Hilo litatokea muda wowote kuanzia sasa na Mwanaspoti limejiridhisha Simba imeanza mazungumzo rasmi ya mbadala wake ambaye ni kipa wa St. Georges ya Ethiopia, Patrick Musotsi Matasi ambaye ni Mkenya.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini imeulizia uwezekano wa kumnunua Manula Simba na viongozi wakamwambia linazungumzika.

Habari zinasema Mamelody wanataka kumsajili Manula kwa vile kipa wao, Mganda Denis Onyango amewaambia anataka kustaafu na hataongeza mkataba tena klabuni hapo kama alivyokwishatangaza nia hiyo kwenye timu ya Taifa.

Hivyo, rada yao kwenye ukanda wa Afrika wameielekeza kwa Manula ambaye mafanikio yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, inafurahisha. Habari kutoka ndani ya Simba zinasema wamekaribisha ofa ya Manula na kutoa angalizo bado ana mkataba wa mwaka mmoja ili wapige pesa ndefu ambayo wana uhakika Wasauzi hao watatoa.

Habari zinasema Simba wameshamseti Matasi ambaye ni nguzo kwenye timu ya Kenya na yuko tayari kuondoka kwani hata Kocha aliyepigwa chini ya Yanga dakika za mwisho, Sebastian Migne naye alishaonyesha nia ya kumleta Yanga.

Simba licha ya kufikiria kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa msimu huu, lakini imepanga pia kufanya biashara ya maana ya mauzo ya wachezaji.

Mbali na Manula pia mtupia mabao wao, Luis Jose ana ofa kadhaa za Sauzi na Morocco ambazo Simba bado wanazicheki kimachale huku wakiendelea kusaka mbadala wa nafasi hizo kimyakimya kabla mkwanja haujaja rasmi mezani.

Ofisa Habari za Simba, Haji Manara ametamba kiwango chao kimataifa kimepandisha thamani za wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.