Mgawo wa CAF wageuka kaa la moto TFF

Mgawo wa CAF wageuka kaa la moto TFF

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amevunja ukimya na kujibu madai yanayolihusisha shirikisho hilo na kifungo cha rais wa Shirikisho la Afrika (CAF), Ahmad Ahmad.

Karia amekwenda mbali zaidi na kudai yuko kwenye mapambano ambayo anaamini atashinda na kuwanyamazisha wanaotamani aanguke kwenye uongozi wake.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) kumfungia kwa miaka mitano Ahmad likimtuhumiwa kwa rushwa, kutoa zawadi na upendeleo, ubadhirifu wa fedha na kutumia vibaya nafasi yake.

Saa kadhaa baada ya hukumu hiyo, TFF ililazimika kutoa ufafanuzi wa taarifa iliyosambaa jana ikihusishwa na mgawo wa malipo yaliyosababisha Ahmad kufungiwa, huku Karia akieleza kuwa kuna watu wana lengo la kutia doa uongozi wake.

Alisema kuwa anaamini katika utendaji bora, hivyo wanaotafuta dosari kwenye utendaji wake wasubiri kushuhudia Tanzania ikifuzu Kombe la Dunia, huku akiwa rais wa TFF. “Watu wanapambana kunichafua lakini hawataweza, hukumu ya Fifa hakuna sehemu wameitaja Tanzania, TFF wala Taifa Stars, hizo ni propaganda ambazo zinatengenezwa na watu lakini hazitafanikiwa.”

Awali, taarifa ya TFF iliyotolewa na ofisa habari, Cliford Ndimbo ilikiri TFF kupokea Dola 100,000 kutoka CAF. “Mei 2017 CAF ilipitisha uamuzi wa kila mwanachama wake kupatiwa fedha hiyo, Dola 80,000 ilipelekwa kwenye maendeleo ya soka na Dola 20,000 ilienda kwa rais wa shirikisho la nchi husika ili kumsaidia kwenye majukumu yake kwa kuwa halipwi mshahara.

“Rais Karia alielekeza Dola 20,000 zitumike kwenye shughuli mbalimbali za shirikisho,” ilisema taarifa hiyo.

By Imani Makongoro na Thomas Ng’itu