Mbeya Kwanza: Yanga wa kawaida, Ngushi aahidi kufunga mabao saba

Muktasari:

  • Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza, ambapo Mbeya Kwanza ndio msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu hivyo kufanya mechi hiyo kuwa ya rekodi na historia.

Mbeya. Wakati Mbeya Kwanza ikiendelea kujifua kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa timu hiyo Harerimana Haruna amesema wanafahamu kuwa wanakutana na timu kubwa, hivyo na wao watacheza kikubwa kupata pointi tatu.

Mchezo baina ya timu hizo unatarajia kupigwa Novemba 30 katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku ikiwa ni mechi ya kwanza kuzikutanisha timu hizo.

Akizungumza Mwanaspoti wakati wa mazoezi yao ya leo asubuhi katika viwanja vya Chuo cha Sayansi na Teknolojia (Must), Haruna amesema Yanga ni timu kubwa hivyo na wao kwakuwa wako Ligi Kuu watafanya mambo makubwa ili kubaki na alama tatu.

Amesema hakuna mechi ndogo kwenye Ligi, huku akichekelea kurejea kwa baadhi ya nyota wake waliokuwa majeruhi akiwamo Nahodha wake, Salum Chuku, Hamis Kanduru na Japheth Majagi aliyekuwa na adhabu ya kadi nyekundu iliyoisha mechi iliyopita dhidi ya Prisons.

"Hatuna presha kwa sababu ni mechi ya kawaida na wapo wachezaji waliowahi kucheza Ligi Kuu hivyo hawaogopi ni kama mechi nyingine tutacheza kawaida tutakuwa makini na wachezaji wote wa Yanga" amesema Haruna.

Kwa upande wake Kipa wa timu hiyo, Hamad Kadedi amesema amejiandaa vyema kuisaidia timu yake huku akifafanua kuwa siyo mara ya kwanza kukutana na mabingwa hao wa kihistoria na kwamba ataongeza umakini ili yasimtokee yaliyomkuta mechi iliyopita aliporuhusu bao la dakika za mwisho dhidi ya Prisons.

"Nimekutana nao Yanga nikiwa Stand United, hivyo sioni presha ila niwaombe wenzangu kila mmoja kuwa makini kutoruhusu hatari kama mechi iliyopita" amesema Kadedi.

Naye Straika na kinara wa mabao kikosini humo, Chrispin Ngushi amesema wako fiti na amejipanga kuwafunga Yanga mabao saba kadri atakapopata nafasi, huku akieleza kuwa wamekuwa wakishindwa kupata matokeo mazuri kipindi cha kwanza jambo ambalo wamelirekebisha.

"Naweza kuwafunga hata mabao saba nikipata nafasi, tumekuwa tukitokea nyuma kusawazisha mabao, hii ilikuwa ni kutokana na ugeni wa Ligi lakini kwa sasa tumezoea hivyo hatutarajii makosa kujirudia" amesema Kinda huyo mwenye mabao matatu hadi sasa.