Mashabiki Simba wateka uwanja wa ndege Songwe wakiwalaki nyota wao

Mbeya. Hii sasa sifa.Ndivyo unaweza kusema kutokana na mamia ya mashabiki wa Simba kutoka matawi zaidi ya 20 waliofurika katika uwanja wa ndege Songwe kuwapokea wachezaji wa timu hiyo wanaotarajia kuwasili muda mchache ujao.

Mashabiki hao wameuteka mkoa wakianzia kwenye hafla fupi ya kupokea makombe ya timu yao kisha kuungana kwa pamoja kuelekea kwenye mapokezi.

Uwanja wa ndege Songwe ulifurika Jezi nyekundu huku shangwe ikitawala viwanjani hapo na kuwafanya wananchi waliokuwa viunga hivyo kubaki na mshangao.

Mwanaspoti ambayo iliwasili mapema uwanjani hapo, ilishuhudia msafara wa magari zaidi ya 10 ukiwa umebeba wafuasi hao wa Wekundu tayari kuwawahi nyota wa timu hiyo.

Simba inashuka jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Jumatatu katika uwanja wa Sokoine.

Mashabiki hao wakiongozwa na viongozi wao wa Mkoa chini ya Mwenyekiti,  Abel Edison waliuteka uwanja huo huku wakitamba kufanya vizuri katika mechi ya Jumatatu.

Mmoja ya viongozi wa Simba kwenye benchi la ufundi walioshuka mapema ni mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally huku akieleza kuwa kikosi kitawasili muda wowote kuanzia sasa.