Mashabiki Simba Mwanza waimaliza Al Ahly mapema

Mashabiki wa Simba jijini Mwanza wakijiandaa kwenda jijini Dar es Salaam kuishangilia timu yao katika mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaochezwa Ijumaa saa 3:00 usiku. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Mashabiki hao wa Simba wameondoka leo Mwanza kwenda Dar es Salaam kuishangilia katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaochezwa Ijumaa, Machi 29, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku

Mwanza. "TUMECHOKA kuishia robo." Ndiyo kauli ya mashabiki wa Simba jijini Mwanza ambao wamefunga safari kwenda Dar es Salaam kuipa nguvu timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, huku wakitamba kuwa mpinzani wao huyo anakufa mabao 4-0.

Simba itacheza na Al Ahly, Ijumaa, Machi 29, mwaka huu kuanzia saa 3:00 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiisaka nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo mashabiki zaidi ya 100 wa timu hiyo wameondoka leo saa 12 jioni kwenda Dar es Salaam kutazama mechi hiyo.

Kaimu Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Mwanza, Salya Ludana amesema huu ni msimu wao wa kuvunja mwiko wa kuishia robo fainali na mashabiki wana morali na ari wa kushuhudia Al Ahly ikitolewa kwa Mkapa.

"Tumeandaa safari hii ambayo tuna magari sita kila moja likibeba mashabiki 30. Matatu yameshatangulia tunafahamu ni mchezo mgumu, lakini tunachotaka Mwarabu asitoke, imani hii tuliyo nayo inatokana na jinsi ambavyo tumeshacheza nao, tunawamudu, tunajiamini na keshokutwa tunawafunga mabao manne," amesema Ludana.

Shabiki wa Simba aliyesafiri kutoka Buchosa wilayani Sengerema, Hamza Habib amesema wameshayajua makosa na kugundua wapi wamekuwa wakikosea, hivyo safari hii wanafanya kweli chini ya kocha Abdelhak Benchinkha ili kufuzu nusu fainali.

"Tumeamua kuungana kwenda kuisapoti timu yetu tunahitaji kuungana kumtoa Mwarabu kwa sababu tuna kikosi kizuri na mwalimu mzuri. Tuna ujasiri mkubwa kuelekea mchezo huu tunamhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan tumejipanga tunakwenda kummaliza Al Ahly," amesema Habib

Naye Winfrida Magoko amesema, "tuna uhakika tumeshajipanga tuna imani tutashinda 4-0, tunaondoka bila hofu kwa sababu tumeshamaliza mipango na tunawaahidi wenzetu kwamba tutarudi na ushindi wao watuombee tufike salama."

Medison Bathlomayo kutoka Kiseke wilayani Ilemela, amesema wamechoka kuitwa mwakarobo kwa sababu ya kuishia robo fainali, hivyo, mwaka huu wamedhamiria kuvunja huo mwiko.

"Tunaamini huu ni msimu wetu wa kwenda nusu fainali tunahitaji mabao mengi kuanzia matatu tumejipanga sawa tuko kamili safari yetu hii siyo bure ina kitu," amesema Bathlomayo

Kwa upande wake, Emmanuel Jileka wa Isamilo amesema: "Nusu fainali tunataka mwisho wa mwarabu ni sasa tumetosha kuishia robo na hawa hawawezi kututisha watakwepa na kuja na kila kitu chao lakini kipigo hawakikwepi tunawafunga kuanzia mabao 3-0."

Mratibu wa mashabiki hao, Nassibu Naimocha amesema lengo la safari hiyo ni kuipa nguvu timu yao na kuhakikisha wanapata pointi tatu kwani zama za Mwarabu zimeshapitwa na wakati na sasa ni wakati wa Simba.

"Tunasafiri kwa sababu tuna uchungu na wachezaji wasicheze kinyonge ili wasiiangushe timu yetu. Tunatumaini kesho mchana tutakuwa Dar es Salaam na safari yetu hii iwe sehemu ya morali kuujaza uwanja na kuwapa nguvu wachezaji wetu," amesema Naimocha