Mashabiki Man United wamkataa Sancho

Muktasari:

Kocha Solskjaer anataka kuboresha safu yake ya ushambuliaji baada ya kwenye dirisha lililopita kuweka mkazo zaidi kwenye ukuta, alipowasajili Harry Maguire na Aaron Wan-Bissaka. Lakini, sasa kinda Mason Greenwood ameanza kuonyesha ubora mkubwa sambamba na Anthony Martial, Marcus Rashford na James - jambo linalowafanya mashabiki wahoji kama Sancho anahitajika.

MANCHESTER, ENGLAND . MASHABIKI wa Manchester United wamemwambia kocha wao Ole Gunnar Solskjaer aachane na mpango wa kumsajili Jadon Sancho kwa sababu Daniel James ni bora zaidi.
Sancho, 19, amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipoondoka Manchester City na kwenda Borussia Dortmund mahali ambako amepewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza tangu mwaka 2017. Lakini, sasa staa huyo anayethamanishwa kuwa na thamani ya Pauni 100 milioni anataka kuondoka kwenye kikosi cha Bundesliga, huku Man United wakitajwa kwamba wanasaka huduma yake kwa nguvu zote.
Kocha Solskjaer anataka kuboresha safu yake ya ushambuliaji baada ya kwenye dirisha lililopita kuweka mkazo zaidi kwenye ukuta, alipowasajili Harry Maguire na Aaron Wan-Bissaka. Lakini, sasa kinda Mason Greenwood ameanza kuonyesha ubora mkubwa sambamba na Anthony Martial, Marcus Rashford na James - jambo linalowafanya mashabiki wahoji kama Sancho anahitajika.
Mmoja aliandika kwenye Twitter: "Sancho hana ubora kumzidi Electric James".
Mwingine aliandika: "Simtaki Sancho, mimi niko sawa tu na James....Hakuna kitu cha spesho kuhusu Sancho...tafadhali tutumie pesa zetu kumsajili Maddison au Kai Havertz."
Shabiki mwingine aliandika: "Sancho anakuzwa tu. Mchukueni Jovic anaweza kucheza pia kama kiungo mbunifu. Atatusaidia kwenye kwenye 4-4-2. Pesa iliyobaki tunasajili beki wa kushoto na Halaand."
Rekodi za wawili hao kwenye ligi mzimu huu, James amecheza mechi 12, ameanza 11, amecheza dakika 984, amefunga mabao matatu, asisti mbili na kupiga mashuti 18, manane yakilenga goli, huku akitengeneza nafasi 11, krosi 43 na kugusa mpira mara 499, wakati Sancho amecheza mechi tisa, ameanzishwa nane, amecheza dakika 666, akifunga mabao matatu na kuasisti matano, akipiga mashuti 14 na manane yamelenga goli, akitengeneza nafasi 14 na kupiga krosi 13 huku akigusa mpira mara 592.