Manula anukia Mamelodi Sundowns

Tuesday April 20 2021
manula pic
By Charles Abel
By Thobias Sebastian

KIWANGO bora cha kipa Aishi Manula katika Ligi ya Mabingwa Afrika kimeivutia Mamelodi Sundowns ya Afrika iliyopanga kuingia sokoni kumnasa ili kwenda kuimarisha safu yao ya ulinzi.

Manula amekuwa nguzo imara kwenye ukuta wa Simba katika michuano mbalimbali, huku msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa katika mechi 10 zikiwamo nne za awali na sita za makundi ameruhusu mabao matatu na kuwa kipa kinara Afrika kwa sasa, jambo linalodaiwa kuwatoa udenda Wasauzi.

Mmoja wa watu wa karibu na Manula amelithibitishia Mwanaspoti kuwa, miamba hiyo ya soka Afrika Kusini inajipanga kumsajili kipa huyo ikimuona kuwa mbadala wa muda mrefu wa kipa wao mkongwe, Dennis Onyango ambaye hivi karibuni atatundika daruga.

“Mamelodi wameonyesha nia ya kumsajili Aishi na tayari wameshaiulizia Simba uwezekano wa kuwauzia. Wao wanataka kumsajili kwa vile wanaona ndiye kipa mwenye umri mdogo anayefanya vizuri kwa sasa, hivyo wanaamini akiongezewa vitu vidogo atakuwa bora na mzuri zaidi ya alivyo sasa,” kilisema chanzo chetu hicho.

“Wanataka Aishi ndiye awe mbadala wa Onyango ambaye tayari ameshawaambia kuwa anajiandaa kustaafu kucheza soka, hivyo kwa vile ametokea hapa Afrika Mashariki (Uganda), wanaona kwamba Manula anaweza kufuata nyayo zake na wanataka kumsajili sasa ili angalau aweze kuzoea mazingira ya timu kabla hajaachiwa mikoba.”

Alisema tayari timu hiyo ya Afrika Kusini imewashawasilisha ofa yao na sasa wanasubiri kuona Simba itaamua nini kwa mahitaji yao juu ya kipa huyo.

Advertisement

Hata hivyo, uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wake, Murtaza Mangungu ulisema kwamba hawajapokea ofa kutoka timu yoyote kumhitaji Manula.

“Hakuna ofa rasmi ya kumhitaji Aishi iliyopo mezani, ila kama itafika, tutakaa chini kujadiliana na kama tutaona inafaa tuko tayari kumruhusu aende. Simba hatuna utamaduni wa kumzuia mchezaji kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama klabu inayomhitaji itatoa ofa stahiki,” alisema Mangungu.

Naye meneja wa mchezaji huyo, Jemedari Said alipoulizwa juu ya taarifa hizo alisema wanaopaswa kuzungumza jambo lolote kuhusu Manula ni Simba ambao bado wana mkataba na kipa huyo.

“Manula ni mchezaji wa Simba na kama kuna ofa wao ndio watatuambia sisi kisha tutakaa kuona kama ina manufaa kwetu au la, hivyo kuhusu hilo suala la Mamelodi nadhani ni vyema mkawauliza wao, ila hadi sasa sisi kwa upande wetu, Simba hawajatuambia chochote,” alisema Jemedari.

Kipa huyo amekuwa ni mmoja kati ya nyota wa Simba waliofanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba wametinga hatua ya robo fainali huku wakiwa vinara wa kundi A.

Katika mechi 10 za mashindano hayo alizocheza msimu huu, amecheza michezo sita bila kuruhusu bao na amefungwa matatu tu - moja dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, kisha kufungwa mawili katika makundi ikiwamo ya ushindi wa 4-1 dhidi ya As Vita na kipigo cha 1-0 cha Al Ahly ya Misri.

Advertisement