Majeruhi wa Al Ahly wampa jeuri kocha Gomes

Sunday February 21 2021
al ahly pic 2
By Oliver Albert

Dar es Salaam. Wakati Al Ahly wakitua nchini usiku wa kuamkia jana, Simba imepata habari njema kutokana na wapinzani wao kuwakosa nyota watano muhimu wa kikosi cha kwanza.

Timu hiyo ya Misri iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ikiwa na kikosi cha wachezaji 22, huku ikiwakosa Ali Maaloul, Taher Mohamed Taher, Walid Soliman, Salah Mohsen na Hussein El-Shahat kwa sababu tofauti.

Nafasi za nyota hao zinatarajiwa kuzibwa na wachezaji Wahid Mahmoud, Mahmoud Kahlaba, Mohamed Magdy, Mohamed Sherif na Ayman Ashraf.

Wakati Ahly wakitua, makocha mbalimbali wa soka wameipa ujanja Simba wa kuwamaliza mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

al ahly pic

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza amewataka Simba kucheza mpira na kushambulia kwa kasi na kamwe wasiruhusu kukaa nyuma muda mwingi kwani wanaweza kuadhibiwa kirahisi na wapinzani wao.

Advertisement

“Wanacheza kitimu, lakini wakikutana na timu ambayo nayo inajua kuchezea mpira kama Simba watapata wakati mgumu. Sasa hapo Simba inatakiwa kutumia hiyo nafasi kucheza mpira muda mwingi, lakini pia wasisahau kujilinda inapobidi.

“Udhaifu ambao niligundua kwa Al Ahly hawako vizuri katika kuzuia mipira ya adhabu, kwani hata katika mechi iliyopita, El Merreikh walipata faulo kama tatu na zilikuwa hatari langoni kwa Al Ahly, hivyo Simba wanatakiwa kulifanyia kazi hilo kwa sababu pia wana watu wazuri wa kumalizia,” alisema Baraza.

Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr alisema kwa jinsi anavyomfahamu kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane, namna nzuri ya kuwabana Al Ahly ni kuhakikisha hawatoi nafasi ya kuwazoea kwenye eneo lao

“Timu ambazo amekuwa akizifundisha Pitso zimekuwa zikipenda kumiliki mpira zaidi ikiwa eneo la wapinzani hiyo inamaana kuwa hutegea wapinzani kujisahau na kuacha nafasi za wao kutengeneza mabao, inahitaji kuwa sawa ili kukabiliana, alinisumbua alipokuwa na Mamelodi,” alisema Kerr.

Advertisement