Kocha Medo aivimbia Simba kibabe

Kocha Medo aivimbia Simba kibabe

Dar es Salaam. Simba inaendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya juzi kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Coastal Union iliyomalizika kwa suluhu.

Katika mechi hiyo, Bernard Morrison ambaye alianza katika kikosi cha kwanza kama beki wa kulia, alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya kiungo wa Coastal (Kante) dakika ya 40, kipindi cha kwanza na kupewa kadi nyekundu.

Morrison alionekana kucheza kwa hasira kama ilivyokuwa kwa wachezaji na kocha wa kikosi hicho, Didier Gomes kutokana na wachezaji wa Coastal kucheza kwa kutumia nguvu zaidi.

Wachezaji wa Simba hawakutaka wala kupenda mpira huo wa kugongana na kutumia nguvu zaidi na muda mwingi walikuwa wakiwapisha Coastal, ambao walikuwa wanacheza kama mechi ya fainali.

Kocha wa Coastal, Melis Medo alisema mechi hiyo na Simba ni kipimo sahihi kwake katika maandalizi yake ya msimu huu kwani wao huenda ndio timu ya kwanza kuanza pre season Agosti 3.

“Wakati huu nahitaji kwanza wachezaji wangu wote kuwa fiti ili tukikutana na timu kubwa yenye wachezaji wabunifu na uwezo binafsi kama hawa wa Simba tuwazuie kwa mwanzo mwisho kama ilivyokuwa katika mechi hiyo,” alisema Medo.