KMC, Polisi TZ patachimbika

WAKIREJEA kutoka ugenini walikoaibishwa kwa kucharazwa bao 1-0 na Kagera Sugar, vijana wa KMC jioni ya leo watawakaribisha maafande wa Polisi Tanzania ambao gari lao limeonekana kuwaka katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, huku kila timu ikijinasibu kuibuka na ushindi.

KMC iliyokuwa kileleni kabla ya kutibuliwa na Kagera, itawaalika Polisi kwenye Uwanja wa Uhuru, huku ikiwa haina kocha wake, Habib Kondo aliyefungiwa mechi tatu kwa makosa ya kinidhamu, imetamba kuendeleza moto walioanza nao msimu huu kabla ya kutibuliwa na vijana wa Mecky Maxime.

Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala alisema kikosi chao kipo fiti kwa mchezo huo na kiu ya vijana wao ni kuendeleza pale walipoishia kwa kuhakikisha wanashinda nyumbani dhidi ya Polisi aliokiri hata hivyo sio timu ya kubezwa kwa matokeo iliyopata kwenye mechi zao zilizopita.

Timu hizo zimetofautiana pointi mbili tu zikiwa zimefuata kwenye msimamo, KMC ikiwa na pointi tisa huku wenzao wakiwa na pointi saba katika mechi nne ambazo kila moja imecheza na kulifanya pambano la leo kuwa gumu na hasa kiu ya safu ya ushambuliaji ya timu hizo.

“Kwa mujibu wa benchi la ufundi, kikosi kipo imara, hatuna majeruhi hata mmoja mpaka sasa na vijana wanaonekana kuwa na ari kubwa kwa mchezo huo, tunaamini utakuwa mchezo mzuri na tutaendeleza pale tulpoishia kwa kuhakikisha tunashinda kwenye uwanja wa nyumbani,” alisema Christina.

Kwa upande wa kocha mkuu wa Polisi, Malale Hamsini, alisema vijana wake wapo tayari kwa mchezo na kiu yao ni kuendelea kupata matokeo mazuri bila kujali wanacheza nyumbani ama ugenini.

Rekodi kwa timu hizo zinaonyesha kwenye msimu uliopita Polisi wakicheza Ligi Kuu baada ya kupanda daraja, iliwatambia wapinzani wao nje ndani kwa kuwafunga mechi zote, nyumbani mabao 2-1 na kushinda tena ugenini 3-2.