Kisinda kutesti mitambo kibabe

Summary

  • Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema Kisinda yupo fiti kukabiliana na timu yoyote sasa kutokana na mazoezi maalum aliyokuwa akiyafanya tangu ametua.

NI wazi sasa kwamba Tuisila Kisinda ataanza kutesti mitambo rasmi kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya timu ngumu na tata, Ruvu Shooting baada ya Mamlaka za Soka kusogeza mbele mechi dhidi ya Ihefu. Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema Kisinda yupo fiti kukabiliana na timu yoyote sasa kutokana na mazoezi maalum aliyokuwa akiyafanya tangu ametua.

Yanga ilipaswa kuwa ugenini dhidi ya Ihefu Septemba 29, lakini sasa wanakutana Novemba 29. Timu hiyo imeganda mkiani mwa msimamo wa ligi huku wao wakishinda tatu na kutoka sare moja.

Nabi ambaye amekwenda kwao fasta kuweka mambo sawa, alisema wachezaji ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa wataendelea na mazoezi kama kawaida kuikabili Ruvu Shooting Jijini Dar es Salaam.

“Tuisila tangu ametua nchini alikuwa na mazoezi maalum chini ya kocha wa viungo anautimamu wa mwili yupo fiti kucheza mechi yoyote iliyo mbele yetu suala la kumtumia au kutokumtumia itategemea na mpango wangu siku hiyo,” alisema na kuongeza;

“Ni mchezaji wa Yanga amesajiliwa ili kuitumikia timu hivyo ni lazima atapangwa. muda ukifika ataonekana akiitumikia timu.”

Alisema ni moja ya wachezaji ambao anawahitaji kwenye kikosi chake kutokana na kasi aliyonayo na sasa amemuaona kuwa ni mchezaji ambaye yupo timamu kimwili kwa mashindano ya kimataifa na ligi ambayo ina mechi nyingi sambamba na Kombe la Shirikisho la Azam anamatumaini makubwa kutoka kwake kwenye suala la kuongeza nguvu.

Akizungumzia Ligi alisema ; “Nina heshimu kila mchezo ulio mbele yangu bila kujali matokeo wanayayapata sasa, nahitaji matokeo ili kuendelea kuwaweka wachezaji kwenye hari nzuri ya ushindani kuelekea michezo yetu ya ligi ya mabingwa.”

Nabi alisema anahitaji matokeo mazuri nyumbani ambayo yatawapa nafasi ya kuendelea hatua inayofuata huku akisisiiza kuona umakini mkubwa eneo la ulinzi wahakikishe hawaruhusu bao.

Yanga ambao wanaanza na Al Hilal ya Sudan wamepania kufanya vizuri kwenye mchezo wa nyumbani ili kuepuka fedheha ya kutolewa mapema kwenye mashindano hayo.

Msimu huu wameonekana kupania kwa kusajili wachezaji wa gharama kubwa na wenye uzoefu wa kimataifa. Uongozi umesisitiza kwamba kila kitu kiko sawa na mashabiki watulie.