Karia aweka sawa udhamini GSM

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) , Wallace Karia.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ametoa kauli juu ya udhamini wa GSM baada ya wadau wengi wa soka kuzungumza mengi juu ya mkataba huo.

Wiki moja nyuma GSM ilisaini mkataba wa miaka miwili na TFF wenye thamani ya Sh 2.1 Bilioni wakiwa kama wadhamini mwenza kwenye Ligi Kuu Bara.

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) uliofanyika jana mjini Morogoro sambamba na uchaguzi mkuu wa Bodi hiyo, Karia alisema udhamini wa GSM ni mzuri tofauti na watu nje wanavyouzungumzia.

“Udhamini wao ni mzuri na sio wamiliki wa timu za Namungo, Coastal wala Yanga, kama ni hivyo basi Yanga wasingeifunga Coastal msimu uliopita lakini waliifunga,” alisema Karia na kuongeza;

“Nafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya klabu za Tanzania ili zipate udhamini, tunatafuta udhamini wa mabasi katika kampuni mbalimbali ili tu timu zipate usafiri.”

Naye Mkurugenzi wa uwekezaji GSM, Injinia Hersi Said alisema: “Sisi ni watu imara na hatuwezi kuyumbishwa na watu wengine, naahidi tupo katika hatua za mwisho kwenye kukamilisha mchakato huu.” Wakati huohuo, Karia alisema wanaona matatizo ya waamuzi na hawatayafumbia macho yale ya makusudi ambayo yatafanywa na baadhi ya waamuzi. “Waamuzi waache kuchezesha kwa uoga, ngumu kuweka VAR kwa sababu gharama za uendeshaji kwa mechi moja wenzetu wanalipa takribani dola 4500 (kama Sh10 milioni),” alisema Karia.

Karia alikiri kwamba mechi nyingi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa zinahusisha wakongwe wa soka nchini Simba na Yanga.