Kangwa wa Azam ana siri nzito

Muktasari:
- Sasa pale Azam FC kuna mchezaji mmoja anayejitofautisha na timu hiyo. Timu inafanya vibaya, lakini anafanya vizuri. Ni Mzimbabwe, Bruce Kangwa.
HUWA inatokea mara chache. Huwa inatokea timu inafanya vibaya halafu mchezaji mmoja anafanya vizuri. Mfano mzuri upo pale Majimaji ya Songea. Timu imechemsha ila Marcel Boniventure anafanya vizuri.
Sasa pale Azam FC kuna mchezaji mmoja anayejitofautisha na timu hiyo. Timu inafanya vibaya, lakini anafanya vizuri. Ni Mzimbabwe, Bruce Kangwa.
Msimu huu amecheza mechi 26 kati ya 27 ambazo timu yake imecheza mpaka sasa. Alikosa mechi ya Mbeya City ya mzunguko wa pili akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na nyota huyo aliyejiunga na Azam miaka miwili iliyopita. Amefunguka mengi.
KIWANGO CHAKE
“Nafasi ya kucheza haipatikani kirahisi, siwezi kusema nina nafasi ya kudumu kisa nimecheza mechi nyingi, kikubwa ni kujituma na kufanya kile ambacho naelekezwa na benchi la ufundi.
Naendelea kupambana kuhakikisha nakuwa katika kiwango bora zaidi, kikubwa ni kujituma tu ili kuendelea vizuri,” anasema Kangwa ambaye ni miongoni mwa nyota waliounda kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe iliyoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana.
“Bado nina mkataba na Azam, sijajua kabisa hatma yangu itakavyokuwa kwasababu Mungu ndiye anapanga, siwezi kusema lolote kwa hivi sasa labda tusubiri. Ninachofanya sasa ni kuzidi kujiimarisha hapa,” anasema.
AWAKUBALI OKWI NA BOCCO
Moto wa washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi na John Bocco waliofunga mabao 34 Ligi Kuu msimu huu haujawaacha watu salama.
Kangwa anakiri kuvutiwa na washambuliaji hao kutoka Simba kutokana na kasi yao ya msimu huu.
“Bocco na Okwi ni wachezaji wazuri hapa, wanajua jinsi ya kupambana na wana nguvu hata katika kuwakaba inabidi utumie nguvu na akili pia kuhakikisha hawakusumbui,” anasema.
AWAPA NENO CHIPUKIZI
Azam msimu huu imekuwa na utitiri wa wachezaji chipukizi ambao walipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Nyota hao ni pamoja na Yahya Zayd, Paul Peter, Shaaban Iddi na wengineo.
Kangwa anasema wachezaji hao chipukizi wanatakiwa kujitambua lakini pia kuwa na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja ili waweze kusonga mbele.
“Vijana wasisubiri mazoezi ya mwalimu ndio wajitume, wanatakiwa wajitume wao wenyewe kwanza halafu mazoezi ya kocha yawe nyongeza. Wasisahau nidhamu ni jambo ambalo wanatakiwa wawe nalo siku zote,” anasema.
AZAM YA SASA
Kiraka huyo Mzimbabwe anakiri kuwa kuna tofauti kati ya Azam ya sasa na ile ya kipindi cha nyuma hasa kwa upande wa wachezaji waliopo.
“Mwanzo walikuwa nyota wengi wazoefu lakini hivi sasa tuna vijana wengi ambao nao wana vipaji vya uhakika ndio maana licha ya kuondoka wazoefu hawa vijana waliopo nao wanajitahidi,” anasema.
Kangwa mwenye motto mmoja wa kiume, Jayden Andrew Kangwa, alisema anataka mwanaye huyo nae acheze mpira ili kurithi kipaji chake.
“Ndio kwanza ana miaka mitatu hivi sasa, napenda sana acheze mpira lakini Mungu huwa anatoa kipaji cha aina tofauti kwa kila mtu, binafsi napenda mwanangu awe anacheza soka,” anasema,
ALITUAJE AZAM
Kangwa anasema alitua Azam baada ya kupelekewa ofa na Wakala wake na kumwambia kwamba kuna timu Tanzania inamuhitaji, hakusita kujiunga nayo bada ya kumwamini vilivyo wakala huyo.
“Zilikuja ofa na zilikuwa nyingi tu mezani lakini wakala wangu aliniambia nitoke, mimi pia nilikuwa nataka nitoke kwahiyo hapo ndio nikajiunga na Azam mpaka leo.”
Baada ya kutua katika kikosi cha Azam, alijikuta katika wakati mgumu hasa upande wa chakula, lakini alijikuta akizoea kula wali na mboga mboga.
“Hakuna chakula kingine ambacho naweza kula hapa zaidi ya wali. Napendelea kutumia mboga mboga muda mwingine supu, mboga zingine zinanishinda,” anasema.
Katika hatua nyingine, beki huyo anasema tangu atue nchini hajawahi kujutia kukaa hapa kutokana na ukarimu ambao amekutana nao kutoka kwa Watanzania.
“Hapa watu wake ni wakarimu sana lakini pia ni marafiki kabisa, lakini mwanzoni mazingira ya yalikuwa yakinitesa ila kadri siku zilivyokuwa zinaenda nikaanza kuzoea, hivi sasa naona kawaida tu,” anasema.