Ishu ya Mwambusi iko hivi

BAADA ya kuibuka sintofahamu ya nini sababu iliyomfanya kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi kujiengua ndani ya kikosi hicho, mwenyewe amelitumia Mwanaspoti kuufafanulia umma wa wanamichezo.

Habari za kuondoka kwa Mwambusi zilianza kuzagaa juzi asubuhi huku kila mmoja akisema lake na wengine wakienda mbali zaidi wakidai kocha mkuu Cedrick Kaze ametaka kocha huyo msaidizi aondoke kwani anataka kufanya kazi na kocha mwingine kijana.

Hata hivyo baadae taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Mshindo Msola ilituliza kidogo hali ya mambo baada ya kubainisha kuwa sababu iliyofanya Mwambusi kujiondoa Yanga ni kutokana na hali yake kiafya kutokuwa nzuri hivyo mwenyewe aliomba kupumzika.

Mwambusi aliiambia Mwanaspoti kuwa; “Niweke wazi kuwa ni kweli hizo taarifa za mimi kupumzika Yanga na yote inatokana na tatizo la kiafya nililonalo ambalo nisingeweza kuendelea kuifanya kazi yangu vizuri.”

“Kuna sehemu ya jino pananiletea maumivu makali jambo linalosababisha kichwa kuuma sana.Sio tatizo la leo wala jana nimekuwa nalo kwa muda mrefu hata miaka miwili imefika lakini nilichukulia kawaida lakini naona hali inazidi kuwa mbaya,” alisema Mwambusi ambaye ni Kocha aliyejenga heshima kubwa akiwa na Mbeya City ile yenyewe.

“Awali nilihisi ni jino labda ndio linaniuma lakini baadae nilivyofanyiwa vipimo ikagundulika kuwa sio jino linalosababisha kichwa kuuma ila kuna mshipa umepita kwenye jino ndio unaniletea maumivu makali sana.

“Baada ya vipimo madaktari wakashauri nifanyiwe upasuaji kwani ndio itakuwa pona yangu hivyo lazima walitoe kwanza jino zima ili kuweza kuokoa huo mshipa uliopita hapo ,”alisema Mwambusi ambaye ameweka rekodi ya kuwa msaidizi wa Makocha wa kigeni akiwemo pia, George Lwandamina na Hans Pluijm kwa miaka tofauti.

Mwambusi ambaye amewahi kuinoa Azam alisema atafanyiwa upasuaji huo Alhamis ijayo kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Hapa nasubiri upasuaji tu na kama ukienda sawa ndio madaktari wataniambia natakiwa kupumzika kwa muda gani na hapo sasa ndio nitajua kama nitarudi mapema kwenye kazi yangu au nitakaa kando muda mrefu ,” alisema Mwambusi.

2013 Msimu ambao Mwambusi aliipandisha Ligi Kuu Bara timu ya Mbeya City na kumaliza nafasi ya nne msimu wao wa kwanza.