Inonga Yanga wanae Desemba 11

Beki wa klabu ya Simba Henock Inonga.
KWA akili ndefu wanazocheza Simba, kwa namna yoyote ile Henock Inonga Yanga wanaye kwenye mechi ya watani Desemba 11 Kwa Mkapa na wajiandae kisaikolojia.
Kumbuka Yanga wao tayari hawatamtumia kiungo wao,Mkongomani Yanick Bangala popote wakimuandaa pia kwa siku hiyo ya Dabi.
Sasa iko hivi; ratiba ya Ligi Kuu Bara inaonyesha Simba wanacheza Desemba Mosi dhidi ya Geita Gold, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkapa ikiwa ni siku mbili mbele baada ya mechi ya Red Arrows kwenye Shirikisho Afrika hatua ya mtoano.
Awali Simba walikuwa na mpango wa kusogeza mbele mechi na Geita kutokana na muingiliano na ugumu wa ratiba kwani baada ya kumalizana nao siku tatu mbele wanatakiwa Zambia kucheza mchezo mwingine wa marudiano na Red Arrows.
Lakini baada ya kikao kizito wakagundua kitu kinachoweza kuwapa ubora zaidi kwenye mechi dhidi ya Yanga ambayo siku hiyo hatumwi mtoto dukani.Wakakubaliana kucheza mechi ya Geita ili beki wake muhimu wa kati, Hennock Inonga Baka kutimiza mchezo wa tatu kutumikia kadi nyekundu ili akipige kwenye mechi ya Dabi dhidi ya Yanga.
Mabingwa hao watetezi wa ligi wamepiga hesabu ndefu kwa kuzingatia upana wa kikosi chao, wakaona kama wasipocheza mechi na Geita maana yake watamkosa Inonga kwenye mechi ya Yanga atakuwa ametumikia adhabu yake mechi mbili tu dhidi ya Namungo na Ruvu Shooting.
Inonga ambaye kabla hajatua Simba wakala wake alishamalizana na Yanga, alisema anaendelea kukiwasha mazoezini na wachezaji wenzake na alisafiri mpaka Mwanza katika mechi ya Ruvu Shooting mbali ya kutokuwepo kwenye mpango wa Kocha kutokana na kadi.
“Tangu nimefika Simba nimeonesha kiwango bora, nitaendelea kufanya hivi ili kuisaidia timu kushinda kila mechi na kuwepo katika kikosi cha kwanza,” alisema Inonga ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na ubora alioonyesha kwenye safu ya ulinzi.
“Kocha amekuja ni mpya naumia kutokuwepo kwenye mechi kwani naamini ningeonyesha kiwango bora zaidi lakini hata mazoezi nitakuwa nimemshawishi na ikitokea akinipa nafasi nitaonyesha kiwango bora.
“Ukiangalia nafasi yetu ina ushindani mkubwa naamini kila ambaye anapata nafasi ya kucheza lengo lake ni kuisaidia timu ndio maana tumekuwa hata tunaelekezana kuanzia mazoezini,”aliongeza staa huyo.
Katika hatua nyingine, kocha wa Simba, Pablo Franco alisema amefurahishwa katika kila nafasi ndani ya kikosi hicho kuna ushindani wa kutosha kwa kila mchezaji ambaye atapata nafasi ya kucheza.
“Kila mchezaji ambaye nimekutana nae hapa amekuwa na uelewa mkubwa katika kunisikiliza na kutimiza majukumu yake ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya kutumia wachezaji hata wale ambao hawakupata nafasi ya kucheza huko nyuma,” alisema Pablo ambaye kwa mujibu wa rekodi zake amefundisha Real Madrid na Getafe za Laliga.
Inonga anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo dhidi ya Coastal Union kwa kumpiga kichwa mchezaji wa timu hiyo ya Tanga ambayo kwenye mechi zake za ugenini tatu wameshinda moja tu na droo moja. Simba imepania kucheza nusufainali ya Afrika msimu huu.