Inonga afunguka mazito Simba

Inonga afunguka mazito Simba

SHIRIKISHO la mpira wa miguu la DR Congo wala halikukosea kumchagua Henock Inonga Baka ‘Varane’ kuwa beki bora wa msimu uliopita kutokana na kiwango bora alichonacho.

Katika mchezo wa dabi dhidi ya Simba miongoni mwa wachezaji waliokuwa katika kiwango bora ni Inonga aliyeifanya safu ya ulinzi ya timu hiyo kuwa salama muda wote alicheza kwa maelewano na Joash Onyango.

Baada ya mechi hiyo kumalizika Inonga alisema mara zote anapokwenda kucheza mechi kubwa kama ile ya Yanga huwa umakini unaongezeka pamoja na kujindaa zaidi ili kuipigania timu.

Alisema mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ni moja ya wachezaji anawafahamu tangu wakiwa DR Congo alijipanga kuhakikisha anamzuia na kutokuleta hatari yoyote.

“Binafsi nilikwenda kutimiza malengo ya kumzuia asifanye hatari yoyote kama ilivyokuwa kwa Heritier Makambo ambaye namfahamu kwani wote tunatoka nchi moja,” alisema Inonga na kuongeza;

“Nafahamu hata mwenyewe anaelewa majukumu ya kazi yangu uwanjani, kama haitoshi ni watu wa karibu ndio maana wakati anatoka nilimtania na baada ya mechi kuisha nilimfuata na kumkumbatia.”

Ikumbukwe Inonga aliletwa nchini na Yanga ambao walimkatia tiketi ya ndege moja na Fiston Mayele wote waje nchini kujiunga na Yanga msimu huu, lakini alipofika kwenye uwanja wa ndege wa Kinshasa, aliwapotea na alikuja nchini siku mbili mbele kujiunga na Simba iliyomsajili kimafia.

Kumkosa Inonga ilithibitika ni pigo kubwa kwa Yanga baada ya juzi beki huyo kuupiga mpira mwingi akionekana kwa wengi kuwa ndiye nyota wa mchezo wa dabi hiyo ya Kariakoo akimtia mfukoni straika wa Yanga, Mayele, ambaye aliamua mechi iliyotangulia ya Ngao ya Jamii.

Inonga alisema anafanya yote hayo kwa ajili ya kuhakikisha timu ya Simba inafanya vizuri kwenye kila mechi ambayo atapata nafasi ya kucheza.

“Nashukuru sana kwa wote ambao wanatambua kazi ambayo nilifanya kwenye mechi ya Yanga kuwazuia washambuliaji wao pamoja na kucheza vile wao wanapenda,” alisema Inonga.

Inonga akishirikiana na Joash Onyango waliinyamazisha safu ya ushambuliaji ya Yanga iliyoundwa na Mayele, Saido Ntibazonkiza, Jesus Moloko na kiungo wa ushambuliaji Feisal Salum.

Inonga alirejea kwa mara ya kwanza juzi kwenye kikosi cha Simba baada ya kukosekana katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara kutokana na kutumikia kadi nyekundu aliyoipata katika mechi ya Coastal Union.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema Inonga alicheza vizuri lakini si vyema kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja sababu wachezaji wote kila mmoja kwa nafasi yake walifanya kazi kubwa.”