Ilemi yaichakaza Itezi michuano ya FA

Thursday November 25 2021
Ilemi PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Mashabiki wa Ilemi FC huenda wasiamke kesho kufuatia timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya ndugu zao, Itezi katika mchezo wa kombe la shirikisho (ASFC) hatua ya kwanza.

Timu hizo ambazo zina upinzani mkali katika Jiji la Mbeya kabla ya mchezo huo tambo zilitawala kwa kila upande ukitamba kuibuka na ushindi ambapo leo Alhamisi ubishi uliisha na mbabe kupatikana.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwa Ilemi 'Timu ya Taifa' kushinda mechi hiyo kutokana na upinzani walioupata dhidi ya wapinzani wao huku wakichagizwa zaidi na mamia ya mashabiki waliofurika uwanjani kushuhudia Chama lao.

Katika kipindi cha kwanza kila timu ilipambana kutafuta mabao lakini washambuliaji wa pande zote walikosa umakini na kujikuta wakienda mapumziko kwa suluhu ya bila kufungana.

Ilemi ilirejea kwa kasi kipindi cha pili na kupata bao kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Itezi, Omary Maziko kuunawa mpira wakati akipambana kuokoa hatari na Gift Leonard kuukwamisha mpira wavuni dakika ya 73.

Katika dakika ya 76, Itezi walijikuta wakibaki pungufu baada ya Nahodha wao, Romalio Soud kuoneshwa kadi nyekundu kufuatia kadi mbili za njano, hatua iliyoweza kuwapa nafasi ya kutawala mechi Ilemi na kuongeza bao la pili kupitia kwa Meshack Samwel dakika ya 80.

Advertisement

Wakati Itezi wakijiuliza, walijikuta wakilazwa bao la tatu lililofungwa na Ramadhan Mhagwa na kuamsha shangwe zaidi kwa mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakishangilia muda wote jukwaani.

Kocha wa Ilemi FC, Josephat Ngole amesema anawapongeza vijana wake kwa kazi nzuri na kwamba kwa sasa wanaenda kujipanga na hatua inayofuata akiahidi kuwa malengo yao ni kufika mbali katika michuano hiyo licha ya kuwa kwenye Ligi ya chini.

Kocha wa Itezi, Ntima Faraja amesema wachezaji wake walitoka mchezoni baada ya mwamuzi kutoa penalti tata kwa wapinzani na kuwafanya kupoteza mwelekeo, huku akidai kuwa hakuzidiwa chochote kumbinu.


Advertisement