Hao kina Samatta hadi wajukuu

Hao kina Samatta hadi wajukuu

PENYE nia pana njia, ndivyo ilivyo kwenye familia ya straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ally Pazi Samatta, kucheza kwake soka kumefungua milango kwa vijana wake hadi wajukuu kufanya kazi hiyo. Mzee huyo alicheza kwa mafanikio makubwa enzi zake, kisha wamekuja vijana wake, huku Mbwana Samatta akifikia levo za juu zaidi kuliko wenzake na sasa mjukuu wake wa tano kati ya 17 tayari ameanza kupata tuzo.

Kujulikana kwa familia hiyo miaka ya sasa, kumetokana na mafanikio ya Samatta kucheza klabu kubwa kama TP Mazemba, Genk ya Ubeligiji, Astone Villa na sasa anacheza kwa mkopo wa mwaka mmoja Fenerbahce ya Uturuki.

Vijana saba wa mzee Samatta wote ni wachezaji kwa ngazi tofauti wa kwanza ni Rajabu aliichezea Polisi Shinyanga ligi ya mkoa, Polisi Tanga, JKT Itende iliopo Mbeya nayo kwa ngazi ya ligi ya mkoa na nafasi yake ni namba 10, ila kwa sasa ni mwalimu wa shule ya msingi ya Aghakhan.

“Kutoka kwenye soka mpaka ualimu ilikuwa hivi, Aghakhan walimuomba kufundisha michezo shuleni kwao baadae akapata nafasi ya kwenda kusomea ualimu na amekuwa mshauri wa michezo katika sekta tofauti,”anasema Mzee Samatta.

Mzee huyo anamtaja kijana wake wa pili kuwa ni Muhsin (No 10) ambaye naye amezichezea timu za 82 Rangers, Shinyanga, Transcup na kazi anayofanya kwa sasa ni sajenti wa jeshi, wakati kijana wake wa tatu Saad, alikuwa nahodha wa Polisi Tanga ligi ya wilaya, Polisi Polisi Mbeya (nahodha), Mbagala market, Ujenzi FC ya Rukwa (nahodha), Polisi Dodoma ambako alibadili namba kutoka 10 akacheza namba tano. Kijana wake wa nne, Said alicheza Kimbagulile na Mbagala Market baada ya kuuzwa na kubadilisha jina kuwa African Lyon, baba yake anaeleza kwamba aliondoka kwenda Afrika Kusini, Mohame (JKT Mgambo), (Mbeya City), (Prisons) na sasa yupo KMC.

Mbwana Samatta ndiye mwenye mafanikio ya juu, ambapo alianza kuichezea Lyon, Simba, TP Mazembe, Genk, Astone Villa na sasa yupo Fenerbahce ya Uturuki ambayo anaichezea kwa mkopo.

Ukiachana na Samatta ambaye ana mafanikio makubwa kuna mdogo wao wa kike anaitwa Sophia, ambaye kamiliza darasa la saba mwaka huu na ameanza pre-form one katika Shule ya Sekondari ya Vikindu yeye anacheza namba tisa.

Mzee Samatta anaelezea siri ya familia nzima kucheza namba 10, kwamba ni ya watu mafundi wa mpira duniani, hivyo anaamini wao wana uwezo wakufanya vitu vikubwa uwanjani.

“Yaani hakuna maana zaidi ya kuvaliwa na mafundi wa soka duniani kama Pele, Diego Armando Maradona, nimeivaa mimi nikicheza Sunderland na Taifa Stars, wameivaa vijana wangu kasoro Mohemed anayecheza namba sita na Sophia mdogo wao anayecheza namba tisa katika timu yake ya Shule ya Sekondari ya Vikindu,”anasema.

Baada ya vijana wake kuonyesha ufundi na baadhi kujikita na majukumu mbalimbali, balaa limeanza kuonekana kwa wajukuu wake ambao wanakuja moto.

Hilary (17) ni mjukuu wake wa tano, aliyezaliwa na kijana wake wa nne kuzaliwa anayeitwa Said, hivi karibuni amekabidhiwa cheti cha heshima cha mchezaji bora wa shule ya Sekondari ya Mbagala.

Alikabidhiwa cheti hicho, baada ya kuhitimu kidato cha nne mwaka huu na sasa anacheza timu ya mtaani kwake inayoitwa Vamsh FC, ambako nako anakuwa anaondoka na zawadi za pesa anazopewa na mashabiki.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Hilary, kujua kipaji chake kilianzia wapi na ndoto yake ipoje, anafunguka mambo mengi, kubwa zaidi anataka kuifikia ndoto ya baba yake mdogo Mbwana anayecheza Fenerbahce ya Uturuki.

“Baba yangu ni Said ambaye ni wanne kuzaliwa kwa babu yangu, alikuwa mchezaji ingawa sijawahi kumshuhudia akicheza, zaidi alikuwa akininunulia mipira ya kuchezea,” anasema.

Anasimulia kuwa, mbali na mipira aliyokuwa akinunuliwa na baba yake, alikuwa anamsimamia katika mazoezi na kwenda kushuhudia baadhi ya mechi alizokuwa anacheza.

“Ukiachana na baba kunifuatilia pia babu amekuwa akinielekeza vitu vingi vyakufanya ili niweze kufika mbali zaidi, kwani anafurahi kuona nacheza namba 10 ya ufundi,”anasema.

SAMATTA ANAMPA SOMO

Anasema baba yake mdogo Samatta, aligundua kipaji chake nakuamua kumpa njia kupita ili aweze kuwa mchezaji mkubwa kwa badae.

“Amewahi kunishuhudia nikicheza baadhi ya mechi, kutokana na kuwa na muda mdogo anapokuja kwenye mapumziko, hawezi kunifuatilia kila wakati, ingawa huwa namtumia video za kazi zangu,” anasema Hilary na anaongeza kuwa,

“Kikubwa ananitaka akili yangu niiruhusu kuwaza vitu vikubwa na kila timu ninayoenda lazima nimtarifu na taratibu zote ninazozifanya huwa anapenda afahamu, anataka nijitume kuliko kubebwa, hilo ni jambo analonisisitiza kila wakati,”anasema. Anasema baada ya kupewa cheti cha heshima ya kuwa mwanasoka bora wa shule, alimtumia kisha akamwambia ndivyo vitu anavyovitaka kuvisikia kutoka kwake. “Aliniambia huo uwe mwanzo, anataka anisikie nikifunga mabao mengi mtaani ambayo yatanitambulisha kutoka kwa wadau wa soka nchini, hivyo napata moyo wa kupambana, nijikifunza kutoka kwa wale walionitangulia kwa maana ya babu na baba zangu,”anasema.


MALENGO YAKE

Hilary anasema anatamani kuanza kucheza soka la kuonekana, licha ya kukiri kwamba si kazi rahisi, hivyo anazingatia ushauri wa baba yake mdogo Samatta, kufanya kitu cha kushitua ambacho kitafanya atazamwe kwa jicho la tatu. “Japokuwa najua baba yangu mdogo atanishika mkono, lakini lazima nifanye kitu ambacho sitakuwa mzigo kwa timu ambazo nitazichezea, nina ndoto kubwa na ipo siku Watanzania, watanijua kwamba ni mjukuu wa mzee Samatta,”anasema.

Pamoja na hilo anafichua kwamba Samatta alimwambia amalize shule ili ajue afanye nini kuhakikisha anakiendeleza kipaji chake.

“Tayari nimemaliza kidato cha nne kwa hiyo, namsubili akikaa sawa najua atanipeleka sehemu sahihi, wakati naendelea kupambana.

BY OLIPA ASSA