Griezmann aambiwa awateme Barcelona
BARCELONA HISPANIA. SUPASTAA, Antoine Griezmann ameambiwa afungashe virago vyake na kuihama Barcelona wakati dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Mwandishi Mfaransa, Frederic Hermel amemwambia fowadi huyo Mfaransa mwenzake, kwamba afikirie tu kusogelea mlango wa kutokea kutokana na maisha yake huko Nou Camp kuwa magumu.
Griezmann amekuwa hana uhusiano mzuri na nahodha wa miamba hiyo ya Catalan, Lionel Messi na chaguo sahihi kwake ni kuondoka tu, kwenda Paris Saint-Germain anakoripotiwa kusakwa akakipige.
Griezmann alijiunga na Barcelona kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana tu hapo akitokea Atletico Madrid kwa ada ya Euro 120 milioni.
Lakini, Hermel aliambia RMC: “Hata rais wa Barcelona anapiga goti anapokuwa mbele ya Messi, ndiye mchezaji wao bora kwenye historia ya klabu ya Barcelona, hivyo ni kawaida.
“Unapowasili kwenye timu hiyo, Messi lazima aamue, yeye anaamua tu muda wake wa kuongeza mkataba. Ataamua kipindi ambacho atataka kuachana na timu hiyo. Lakini, ukweli hakuna muunganiko baina ya wawili hao, Messi na Griezmann.
“Hilo linafanya Griezmann awe kama mfu Barcelona, anajaribu kufanya kila kitu na pengine akubaki tu kutumika kwenye dili la kumrudisha Neymar hapo, ili yeye aende PSG.”