Fiston aibua mapya Yanga

STRAIKA wa Yanga, Waziri Junior amecheki upepo unavyokwenda akamwambia Kocha Cedrick Kaze amuachie akatafute maisha mbele kwa mbele. Lakini Kaze akamwambia, “huendi kokote, najua cha kufanya.”

Waziri mpaka sasa amefunga bao moja pekee katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara alizocheza akiwa na timu hiyo, lakini Kaze ameonekana kuendelea kumwamini zaidi kuwepo kikosi kwake ingawa yupo tayari kwenda kusaka changamoto mpya sehemu nyingine.

Waziri amekuwa na wakati mgumu mbele ya Michael Sarpong ambaye ndiye hutumika mara kwa mara na sasa Yanga imesajili straika mwingine, Fiston Abdulrazak Fiston raia wa Burundi ambaye amezidi kumchanganya Waziri kwani anaona nafasi imezidi kuwa finyu. Kwa usajili huo, Waziri anapaswa kupambana zaidi ili kuendelea kumshawishi kocha wake japo kumpanga kikosini katika mechi zilizobaki za ligi pamoja na mechi za Kombe la Shirikisho la Azam.

Yanga ilimsajili Waziri aliyekuwa amefunga mabao 13 msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mbao FC iliyoshuka daraja, lakini hana nafasi kwenye kikosi cha Yanga ambacho kimecheza mechi 18 na kukusanya pointi 44 zilizowaweka kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Waziri alisema kuwa alikuwa na malengo makubwa baada ya kutua Yanga, lakini hayajatimia kutokana na kutopata nafasi ya kucheza ingawa kocha wake amekuwa akimtia moyo wa kupambana.

Alisema kuwa hata wakati wa dirisha dogo, kuna baadhi ya timu zilimhitaji kwa mkopo, lakini jambo hilo kocha alilikataa kutokana na kuonyesha kuwa bado anahitaji uwepo wake ndani ya timu hiyo.

“Raha ya mpira ni kucheza, huwa nafurahi sana kucheza kuliko kitu kingine, ili mchezaji acheze ni lazima kocha ndiye apange nani atamtumia, hivyo naamini wakati wangu wa kucheza utafika,” alisema Waziri.

“Nilitamani kuwa mfungaji bora nilipotua Yanga kwani kabla sijatua nilikuwa mfungaji wa pili nyuma ya Kagere wa Simba, hivyo niliamini kabisa kuwa nitaweza na sijakata tamaa ingawa msimu huu kuna kuchangamoto na kutimiza lengo haitawezekana.

“Naamini nipo kwenye mipango ya kocha wangu, ndiyo maana hata timu zingine ziliponihitaji kwa mkopo alikataa, hivyo naendelea kujituma ili kupambania namba kama alivyowahi kuniamini kwenye mechi tatu nilizocheza, ila huko mbele wakiruhusu niende kwa mkopo nipo tayari.”

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu kadhaa kama Simba, Azam FC na Mbao FC ambayo ilikuwa timu yake ya mwisho kabla ya kutua Yanga, alisema kuwa anaamini kila mchezaji ndani ya timu hiyo ana mchango wake, hivyo hata wanaokosa nafasi ya kucheza tofauti yao sio kubwa.

“Kama nilivyosema hakuna asiyependa kucheza, ila hatuwezi tukacheza wote kwa wakati mmoja, hivyo kila mmoja atacheza kwa wakati wake ukifika, Yanga imesajili wachezaji wazuri ambao lazima wapambane kupata kile ambacho timu inahitaji.

“Ni kweli usipopata nafasi mara nyingi kucheza kiwango kinashuka, binafsi huwa nalinda kiwango changu kwa kufanya mazoezi hata nje ya timu ili nikipata nafasi nifanye nitakachoelekezwa ingawa sitakuwa sawa kiwango na wale wanaocheza mara kwa mara.”