FANTASTIC FOUR: Ole yupo bize na vichwa vinne

MANCHESTER ENGLAND. NDO hivyo. Lisemwalo ni kwamba Manchester United imeorodhesha safu ya washambuliaji wanne akiwamo supastaa wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho kwamba ndio watakaopambana mchana na usiku kunasa saini zao katika dirisha lijalo la usajili.

Man United chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer inatarajia kuwa bize wakati dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa licha ya kuripotiwa kuwapo kwa hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga la corona, ambalo limeziathiri klabu nyingi za soka.

Kwa mujibu wa ESPN, Sancho bado anapewa kipaumbele kikubwa cha kunaswa na mabingwa hao mara 20 wa England, lakini wakali wengine Jack Grealish wa Aston Villa, Moussa Dembele wa Olympique Lyon na Timo Werner wa RB Leipzig ni washambuliaji waliopo kwenye orodha ya wanaowindwa kwa udi na uvumba huko Old Trafford.

Jambo hilo la kuhusishwa na kuhama kwa staa Sancho limeanza kuzingatiwa na miamba ya Ujerumani, Dortmund ambapo kwa sasa wamekuwa wakimwaanzishia benchi Mwingereza huyo tangu msimu wa Bundesliga uliporejea katikati ya Mei.

Mastaa Grealish na Dembele nao wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kuzihama timu zao, Aston Villa na Lyon mtawalia kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, huku Werner naye maisha yake yamekuwa yakiandamwa na uvumi wa aina hiyo siku za karibuni. Liverpool wamekuwa wakihusishwa sana na kutaka saini ya straika huyo wa RB Leipzig, lakini imeelezwa kwamba janga la corona limetikisa timu nyingi kiuchumi na jambo hilo linaweza kuwabana wakali hao wa Anfield wakashindwa kuwa na pesa inayotosha kunasa huduma ya Mjerumani huyo aje kwenye timu yake kwa ajili ya msimu ujao wa 2020-21. Man United ilimsajili straika Odion Ighalo kwa mkopo dirisha la Januari akitokea Shanghai Shenhua, lakini mpango wao ni kuingia sokoni kutafuta mrithi wa Romelu Lukaku, ambaye iliimuza kwenda Inter Milan.