Fainali Europa Baku inavyoacha maswali mengi

Muktasari:

  • Arsenal na Chelsea – zote za jijini hapa London, zimesonga hadi fainali ya Ligi ya Europa ambayo imepangwa kufanyika Baku, Azerbaijan. Ni huko watu wanakonyooshea vidole na kufungua ramani kujua Baku inapatikana wapi.

KUNA baadhi ya mambo hata watoto wadogo au wasiokuwa watu wa mpira wakisikia lazima asilimia yao kubwa watatia swali, kutokana na utata wenyewe.

Mwaka huu timu nne za England zimefanikiwa kufika fainali za mashindano makubwa Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa moja kufanya hivyo.

Liverpool na Tottenham Hotspur wamefanikiwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), itakayochezwa Madrid, Hispania. Hiyo haina shida.

Arsenal na Chelsea – zote za jijini hapa London, zimesonga hadi fainali ya Ligi ya Europa ambayo imepangwa kufanyika Baku, Azerbaijan. Ni huko watu wanakonyooshea vidole na kufungua ramani kujua Baku inapatikana wapi.

Timu zote zinatoka hapa London, zipande ndege na kusafiri umbali wa maili zaidi ya 5,000 kwenda kuutafuta Uwanja wa Olimpiki ulioko Baku, huku uwanja wa ndege ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 15,000 tu kwa siku, tena safari ni za kuungaunga na fadhaa yake ni ya kufa mtu.

Unabaki kujiuliza Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) lilikuwa na masilahi gani hadi kupeleka mechi kubwa kiasi hiki huko? Je, kuna timu inatoka upande huo ilitarajiwa kufika fainali kwa hiyo labda ni moja ya njia za kuvutia soka na kuikuza huko? Hapana.

Ikiwa mazingira yenyewe ndiyo hayo kiusafiri na kiumbali, mmoja atafikiria kipi zaidi? Bila shaka atazama kujiuliza hii ni nchi ya aina gani, watu wake wakoje, watawala na rekodi zinasema nini.

Kabla hatujaenda huko, ieleweke kwamba pamoja na Uefa kuwa wakisema sera yao ni kuzungusha fainali kutoka nchi au mji mmoja kwenda mwingine, hakuna ubishi kwamba tiketi ya dhahabu kama hii lazima itolewe kwa sababu kubwa na za kuridhisha.

Baada tu ya wana fainali kubainika, Uefa wameshabanwa na kuomba radhi kubwa kwa Arsenal waliowatandika barua, na sasa wanasema wanaomba ushirikiano ili wawasaidie mashabiki kufika huko pasipo matatizo. Kila timu ilitengewa tiketi 6,000 hivi lakini karibu nusu zinarudishwa kwa sababu ya taabu ya safari hiyo, ambapo kwa kifupi ili mmoja awe salama kazini au kwenye biashara yake, lazima atenge na kupanga vyema walau siku nane kwa ajili ya kwenda, kuona, kurudi na kujiandaa kurejea ‘mzigoni’.

Nani ana muda wa hivyo nyakati hizi? Ajabu ni kwamba uamuzi wa kuwapa Baku uenyeji ulifanywa Septemba mwaka juzi, yaani 2017, wiki chache tu baada ya kuanza kuibuka au kuwekwa wazi kwa kashfa mbalimbali juu ya taifa hili kimataifa, ikiwa ni pamoja na uozo wa ndani mwake na jinsi wanavyofunika kombe mwanaharamu apite au kuhakikisha uchafu unabaki ndani ya zulia.

Siyo muda mrefu, labda tutapokea hayo matangazo kutoka huko ikiwa utakuwapo mwanga na kujua nani anakuwa mwamba zaidi hiyo Mei 29 baina ya watani wa jadi wa England – The Blues na The Gunners. Uwanja wao ulijengwa kwa ajili ya Michuano ya Ulaya 2015.

Huenda Azerbaijan haimaanishi makubwa wala mengi kwako; magharibi pengine zaidi kwa washindi wa nyimbo wanaozifanya katika mazingira magumu au labda ushindi laini kwa ajili ya mashindano mengine ya soka ya kimataifa.

Ni moja ya zile Jamhuri za Kisovieti za Kisoshalist za Urusi kabla ya kuja kujitenga na pia ni wanapakana na Iran kwenye moja ya mipaka yake.

Wana mafuta, kwenye ukanda wa ufukwe wa Bahari ya Caspian na watu wake ni milioni 10. Lakini kuna upande mwingine; uandishi wa habari ni kana kwamba ni jinai nchini humo – takwimu zipo wazi; watu 10 kati ya wafungwa wa kisiasa 158 ni wanahabari. Shirika huru la mwisho la habari nchini Azerbaijan limefungwa wiki jana. Gharama ya kukaidi maelekezo ya watawala ni kubwa. Askari kanzu wamekuwa na kazi kubwa ya kufuatilia watu, kuwapiga picha hapa na pale, kuwarekodi na ikiwa ubishi unazidi ni kutupwa ndani tu.

Kuna taarifa zilizovuja; za zaidi ya mwaka mmoja uliopita, zikionesha kashfa kubwa zinazoihusisha Uingereza na taifa hilo – utakatishaji fedha wa pauni bilioni tatu hivi pamoja na uwapo wa kile kinachoitwa utetezi na ushawishi, ambapo waliolamba mpunga huo ni pamoja na wanasiasa na waandishi wasiojali maadili.

Inaelezwa sehemu ya fedha imekuwa inakwenda kwa ajili ya kumsafisha Rais dikteta, Ilham Aliyev na mkewe Mehriban ambao wamekuwa wakiishi katika pepo yao. Japokuwa nchi imeondolewa kwenye umasikini uliokithiri, bado ni tegemezi kwenye mafuta tu bila kuwa na ubunifu mwingine unawaweka pabaya.

Watawala wa Azerbaijan, wanadai kwamba waliendesha mradi wa siri kwa ajili ya malipo kwa Wazungu maarufu na wenye ushawishi, kuwanunulia bidhaa ghali na za anasa, kutakatisha fedha kupitia mtandao wa kampuni za siri za Uingereza, ikielezwa kitita kilifikia Pauni 2.2 bilioni. Rais huyo amekuwa England na alipiga picha hata akiwa 10 Downing Street.

Takwimu zilizovuja na kupatikana zinaonyesha utawala wa Baku unatuhumiwa kukiuka na kukandamiza mno haki za binadamu, wakihakikisha mfumo wenyewe ni wa kifisadi kwa ajili ya kuhujumu uchumi na kuhakikisha kura zinaibwa kwa upande wao na kwamba kati ya 2012 na 2014, malipo makubwa ya siri na yasiyokatiwa stakabadhi, walau za mikono tu, yalifanyika mara 16,000 na hakuna anayethubutu kuhoji.

Inaelezwa kuna kampuni ya Kiskochi inayotumiwa kutelezesha fedha hizo kutoka Baku hadi Uingereza.

Hiyo ndiyo Baku, huko ndiko Azerbaijan ambako Arsenal na Chelsea wanakwenda kucheza fainali ya Kombe la Europa.

Sababu hadi leo haijatolewa ya fainali kupelekwa huko, lakini radhi imeombwa kwamba utakuwa usumbufu na kwamba haikutarajiwa fainali ingekutanisha timu zote za England.