Dube amekuja kuwashika!

BAADA ya kusota kwa siku 273 bila kutikisa nyavu hatimaye mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ametoa gundu kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United unaopigwa kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Dube alimaliza na mabao 14 msimu uliopita, akiwa kinara wa timu yake licha ya kutumia muda mrefu nje ya uwanja kujiuguza majeraha na mara ya mwisho kufunga ilikuwa Mei 20 mwaka jana dhidi ya Biashara United.
Ijumaa iliyopita Mzimbabwe huyo aliyeshiriki Fainali za Afcon 2021 zilizofanyika Cameroon, alifunga bao wakati Azam ikiinyoosha Pamba kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa Nyamagana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya kesho dhidi ya Biashara, timu aliyoitungua mara ya mwis ho katika Ligi Kuu.
Azam na Biashara zitaumana CCM Kirumba baada ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, uliopo Musoma mkoani Mara kufungiwa kutokana na kukosa vigezo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Dube alisema amekaa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ila anafahamu kilichomleta ndani ya timu hiyo kuwa ni kufunga hivyo ni muda wake sasa.
“Nafurahi kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoleta furaha ndani ya timu nimefunga hiyo ndio kazi yangu nikipewa nafasi zaidi nitafunga na nitakuwa miongoni mwa wachezaji watakaofunga mabao mengi msimu huu kwa sababu ndio kazi iliyonitoa Zimbabwe na kunileta Tanzania,” alisema Dube na kuongeza;
“Hakuna kitu kinaumiza kuwa nje kwa majeraha.”