Chama aiwahi Yanga Kirumba

Chama aiwahi Yanga Kirumba

BAADA ya kupata sare kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam, kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba kitaondoka Dar es Salaam jioni ya leo kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo na Geita Gold Mei 22.

Msafara wa Simba unatarajiwa kuondoka na wachezaji wote hadi Clatous Chama kwani baada ya kumalizana na Geita wataweka kambi mkoani humo kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ASFC dhidi ya Yanga Mei 28.

Chama bado hajawa fiti lakini Simba wanakwenda naye kuangalia fitinesi yake na lolote linaweza kutokea kutokana na umuhimu wa mchezo huo wa watani.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema wamepania kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa kwenye mzuka wa aina yake na wapate kitu mkononi.

Pablo alisema kulingana na ukubwa wa Simba ulivyo aina ya mashindano wanayoshiriki anahitaji kuona kila mchezaji anakuwa kwenye ubora ikiwemo kwenye mechi za ligi na ile ya Yanga ila kuna wengine wamekuwa wakishindwa kufanya hivyo.

Alisema mechi dhidi ya Azam walikuwa na makosa yaleyale ya kutengeneza nafasi za kufunga mabao ila wamekuwa wakishindwa kutumia kuzigeuza kuwa mabao.

“Kuna namna tunatakiwa kuweka nguvu na kuendelea kurekebisha hilo, bado tupo kwenye mashindano hakuna cha kufanya zaidi ya kupambana kwa kuwatumia wachezaji waliopo ili tufanye vizuri kwenye mechi zijazo.

“Msimu ukimalizika tunaweza kupata muda wa kuboresha kikosi chetu kwa kuangalia njia gani sahihi tunaweza kutumia ili kupata wachezaji bora na kuona tunafanya vizuti zaidi,” alisema.

“Tumeandaa timu ili kuona tunashinda ila kwenye mpira matarajio yanaweza kuwa tofauti kulingana na maandalizi yako hilo tumekutana nalo sana kwa upande wetu msimu huu,” alisema Pablo na kuongeza;

“Kuhusu ubingwa wa ligi kwa upande wetu baada ya matokeo haya dhidi ya Azam inategemea vinara wa ligi Yanga watakuwa wanapata matokeo gani katika michezo yao iliyobaki.”

Simba ina pointi 50, kumi nyuma ya vinara Yanga.