Bosnia azikwa, Ummy amlilia

Bosnia azikwa, Ummy amlilia

Tanga. Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu na nyota wa zamani wa soka nchini ni miongoni mwa waombolezaji waliomlilia aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa African Sport, Abdul Ahmed ‘Bosnia’ aliyefariki dunia juzi jijiji Dar es salaam kwa kushambuliwa.

Wakizungumza katika maziko hayo, walisema Bosnia ameondoka katika kipindi ambacho mchango wake ulikuwa ukihitajika katika timu yake ya Africn Sport na Mkoa wa Tanga katika kuongoza mikakati ya kuipandisha daraja.

Ummy alisema Bosnia ameacha pengo kubwa katika medani ya soka jijini Tanga kwa sababu alikuwa akishirikiana naye kwa karibu na walishaweka mikakati thabiti ya kuhakikisha African Sport inarejea katika ubora wake wa miaka ya nyuma.

“Nimeguswa mno na kifo chake, niahidi tu kuwa nitahakikisha waliohusika na mauaji yake wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Ummy.

Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Dougras Muhani alisema Bosnia ameacha pengo kubwa la kiuongozi na utawala na kuwataka wachezaji wa African Sport kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao cha majonzi.

“Bosnia alikuwa kiungo wa kuiunganisha African Sport na wadau wengine wa michezo, kifo chake kimetuduwaza, lakini hiyo ni kazi ya Mungu hatuwezi kuikosoa, tunachohitajika kufanya sasa ni kumuombea Mungu ampumzishe mahala salama,” alisema Juma Mgunda, ni kocha wa Coastal Union.

Abdul Ahmed aliyezaliwa 1971, alizikwa jana saa 7 mchana katika makaburi ya familia yake yaliyopo Mwambani, jijini Tanga, akiwa ameacha mke na watoto watano.

Kabla ya kuwa kiongozi katika klabu hiyo, Bosnia alikuwa mchezaji akichezea nafasi ya ushambuliaji katika timu hiyo iliyompatia umaarufu.

Umauti umlimkuta mwanamichezo huyo akiwa Dar es Salaam na timu yake ya African Sports, ambayo Jumatatu ilikuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.

_____________________________________________________________

 By Burhani Yakub