Boma waendeleza uteja kwa Tunduru Korosho

Friday November 26 2021
Boma PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Tunduru Korosho imeendeleza ubabe kwa Boma baada ya leo Ijumaa kuichapa bao 1-0 katika mchezo wa kombe la shirikisho (ASFC) hatua ya kwanza ulipigwa uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kipigo hicho kwa Boma kinakuwa cha pili dhidi ya wapinzani hao baada ya mechi iliyowakutanisha kwenye Ligi kukubali kipondo cha mabao 3-0 katika uwanja huo.

Katika mchezo wa leo ilishuhudiwa soka safi na la kuvutia kwa timu zote, lakini Boma walionekana kuumudu  mpira lakini ishu ilikuwa ni kupata mabao.

Boma walitengeneza nafasi zaidi ya nne wakiingia eneo la 18 kwa wapinzani lakini bahati haikuwa upande wao haswa kipindi cha kwanza na kumaliza dakika 45 za awali kutoshana nguvu bila kufungana.

Tunduru Korosho walicheza kwa mashambulizi ya kushtukiza na dakika ya 62 Eliya Haruna akaipatia bao kwa shuti kali nje ya 18 na kudumu hadi dakika 90 za mpambano huo.

Hata hivyo ishu ya uwanja ilionekana kuwapa shida wachezaji wa timu zote kutokana na kuharibu mipango kutokana na utelezi kufuatia  mvua iliyonyesha mapema kabla ya mechi.

Advertisement

Kocha wa Tunduru Korosho, Kesy Mzirai amesema licha ya upinzani walioupata kwa wenyeji lakini wameweza kufikia malengo na kwamba wanaenda kujipanga na hatua inayofuata.

"Wapinzani walijipanga lakini walikuta na sisi tuko fiti na imara mwisho wa mechi tukaweza kuondoka na ushindi na sasa tunajipanga na hatua nyingine kukutana na yeyote" ametamba Mzirai Kocha wa Tunduru Korosho.

Naye Kocha wa Boma FC, Joel Ipanda amesema changamoto waliyoipata ni kutokuwapo maamuzi rafiki kwa mwamuzi wa mchezo huo na kwamba pamoja na kupoteza lakini mpira wameupiga.

"Mpira tumeucheza ila mwamuzi kaamua alivyotaka, niwapongeze vijana wangu kwa kazi nzuri huenda haikuwa bahati yetu na mapungufu yaliyoonekana tutayafanyia kazi" amesema Ipanda.

Advertisement