Barbara yamemkuta huko, akamatwa na Polisi

OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amedai kuwa kuna mambo yanaendelea kwenye sakata lake la kukamatwa na Jeshi la Polisi Januari 20 na kukaa ndani kwa masaa nane akituhumiwa kutoa lugha chafu kwa mmoja wa maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Barbara aliliambia Mwanaspoti kuwa anahisi kuna vita ya kimpira inaendelea chini kwa chini ili kumdhohofisha. Alidai Alhamisi asubuhi akijiandaa alipigiwa simu na Polisi ambao walimtaka afike Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, siku hiyo kwa kuwa amefunguliwa kesi.
“Mimi niliwajibu mbona kesi ilifunguliwa na kufungwa kwa sababu hakukuwa na chochote, wakaniambia hapana nimefunguliwa kesi ya jinai kwamba nimetumia lugha chafu ya matusi, baada ya kauli ile ilinibidi nienda ila cha kushangaza nilipofika nilishikiliwa polisi masaa nane,” alisema Barbara kwenye mahojiano na Mwanaspoti na kuongeza:
“Kiukweli jambo hili limenistua na kuniumiza, hiyo siku nilijiuliza sana niwaambie watu nikasema ngoja niache kwanza mechi ya Mtibwa Sugar ipite, ila nilianza kuwatafuta viongozi wa Bodi ya Ligi na TFF ili niwaeleze kuhusu uwanja wakawa wanakata simu zangu,”alisema ingawa jana mchana, TFF walitoa tamko kukana kuhusika na kesi yoyote iliyoko Polisi.
“Nilijiuliza kusema neno stu..d (upuuzi) na nonsense (ujinga au haina maana) imekuwa leo hii ndio matusi, wakaniambia unajua nilikosea napaswa kuwajibika, hivyo wanahitaji vifaa vyangu vyote kwakuwa wanaendelea na uchunguzi na nisipowapa ushirikiano watanifuata hadi nyumbani.
“Kiukweli ilikuwa ni kitu kikubwa yaani hadi sasa hivi kisaikolojia hata siko sawa na sijatulia kabisa, hii vita sasa imekuwa kubwa na imefika pabaya.
“Wanafanya hayo ili kunirudisha nyuma nisifanya kile ninachotaka kufanya, fikiria leo unamkamata CEO nakumuweka ndani nia yao ilikuwa nilale ndani kule, kiukweli hii imeniumiza na ninaona hawa watu hawana nia njema kabisa.”
Alipotafutwa na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema: “Sina taarifa hzio mimi nd’o kwanza nakusikia wewe unaniambia kama kuna ishu kama hiyo.”
Akijibu juu hilo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo alisema: “Taarifa inayosambazwa kuonyesha TFF imefanya hivyo ni za upotoshaji wenye nia ovu. Tunawataka wote wanaoendesha propaganda hizo kuacha mara moja. TFF haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaoendelea kuzisambaza.”