Aussems awaza ubingwa

Aussems awaza ubingwa

KOCHA wa AFC Leopards, Patrick Aussems kasema msimu ujao anapania kuifukuzia taji la Ligi Kuu baada ya kutumia msimu huu, kusuka kikosi kipya kabisa.

Hii ni kufuatia Ingwe kupoteza wachezaji 11 tegemeo wa msimu uliopita na kumlazimu Aussems kuanza upya. Lakini Aussems anasisitiza kwamba licha ya kuwa kikosi kipya alichokisuka kimeshika nare, atahitaji sapoti kubwa kutoka kwa uongozi wa klabu hasa kwenye suala la kujali maslahi ya wachezaji wake.

Hii itasaidia kwa kuhakikisha hawatorokwi tena na wachezaji. Sasa naye mwenyekiti wa Ingwe Shikanda kamjibu kwa kufafanua mipango aliyonayo ya kuistawisha Ingwe kuanzia msimu ujao ili kuhakikisha wanapunguza hali yao ya msoto.

Mara si moja, uongozi wake umeshtumiwa na Aussems kwa kushindwa kujali maslahi ya wachezaji.

Wachezaji Ingwe kwa sasa, wana zaidi ya miezi mitatu toka walipolipwa mshahara wao wa mwisho.

“Nilipochaguliwa, kipaumbele ilikuwa kuweka mikakati bora ya kuistwisha klabu na wala haikuwa kuboresha matokeo. Kuwawezesha wachezaji bila ya kuiwezesha klabu haitasaidia. Mchezaji akiwa bora atavutiwa na klabu nyingine na ataondoka ila klabu itabakia pale pale. Sasa kuistawisha klabu kwanza ndilo la msingi na muhimu sana kwangu,” Shikanda kamjibu.

Kando na kuandaa michango kadhaa, Shikanda analenga kutengenza sajili mpya ya mashabiki, kusaka wadhamini zaidi na wa muda mrefu pamoja na kupunguza matumizi ndani ya klabu.