Aucho na Mukoko ni vita Yanga

Aucho na Mukoko ni vita Yanga

UFUNDI aliouonyesha Khalid Aucho katika dakika 360 alizocheza,zinampa wakati mgumu, Mkongomani, Tonombe Mukoko kuwa na kazi ya ziada lakini wadau wamesifia ushindani wao Yanga.

Dakika 360 za Aucho zimepatikana katika mechi nne alizocheza dakika zote 90 kila mechi akianza na Kagera Sugar, Geita Gold, KMC na Azam FC na kwenye michezo hiyo timu yake imepata ushindi, pia amemudu kucheza na viungo wenzake aliocheza nao.

Tofauti na Mukoko anakuwa mzuri zaidi akicheza na Feisal Salum’Fei Toto’ ambao ndio walikuwa injini ya timu msimu uliopita tofauti na sasa kwa Mukoko ambaye imethibitika kuwa anajua kutafuta mpira kuurudisha kwenye himaya yao.

Jambo ambalo linampa ujiko Aucho ambaye ni mzuri zaidi timu ikiwa na mpira,anakaba, anatoa pasi za utulivu.

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Milambo, alisema; “Aucho kwanza ni mchezaji mwenye uzoefu na amecheza michezo mingi ya kimashindano ni mchezaji ambaye anaufanya mpira kuwa rahisi kutokana na namna yake ya uchezaji.”

“Ni mchezaji ambaye ni mwalimu kiwanjani na anajua ni muda gani atoe pasi muda gani abaki na mpira mguuni ili kuhakikisha anatoa kitu kwa uhakika na kinafika kwa mtu anayemkusudia hana presha,” alisema.

“Huyu Mukoko ni mzuri wakati timu haina mpira lakini timu ikiwa na mpira hana umiliki mzuri wa mpira kwanini timu ikiwa na mpira amekuwa akikaba kuutafuta.”

Naye Akida Makunda alisema ubora wa Aucho unachangiwa na uelewano na Bangala wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa.