Ally Mayay akubali yaishe

Aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi Wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mayay amesema sio lazima awe kiongozi hivyo kilichomtokea kwake anakiacha kama kilivyo na hakitamrudisha nyuma katika kupigania maendeleo ya soka hapa nchini.
Mayay ni mmoja ya wagombea urais aliyeenguliwa na kamati ya uchaguzi ya TFF kwa kukosa baadhi ya sifa ikiwemo kukosa wadhamini watano.
Mayay ameenguliwa katika nafasi hiyo pamoja na wengine wawili ambao ni Ally Saleh na Oscar Oscar.
Mchezaji huyo wa zamani Wa Yanga na Taifa Stars amesema maendeleo hayaji bila changamoto iwe ya kumuumiza mtu au kumjenga hivyo hicho kilichomtokea hakiwezi kumyumbisha vali ataendela kupambania maendeleo ya soka nchi hasa katika kuwasaidia wachezaji.
"Sio lazima niwe kiongozi ili kusaidia mpira ili mradi Mimi ni mwanafamilia wa mpira wa miguu na nina uzoefu nitaendela kusaidia wachezaji kulingana na nafasi yangu kadri Mungu atakaponijalia uhai," amesema Mayay.
Mayay amesema kwenye upande wa wadhamini ni kweli alipeleka mdhamini mmoja lakini kwenye vyeti alipeleka vyeti
Halisi lakini akakiri havikuhakikiwa.
"Kwenye wadhamini nilijianga muda mrefu kwa kufanya jitihada kubwa za kuongea na wenyeviti na makatibu wa mikoa zaidi ya 21 pamoja na klabu 18 lakini nikaambulia mdhamini mmoja tu na siwezi kulaumu kwani ni matakwa yao, huwezi kumlazimisha mtu.
" Kuhusu kitambulisho cha uraia pamoja na vyeti vyote nilipeleka halisi (original), na kweli havikuwa na fomu ya saini kuonyesha kuwa vimehakikiwa lakini tulizungumza kwenye usaili jambo hilo, kwamba siwezi kupeleka vyeti feki pale kwani si ingekuwa kesi ," amesema Mayay.