#WC2018: Ronaldo auota ubingwa Kombe la Dunia 2022
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo Real Madrid mwenye miaka 33 aliyetarajiwa kuipa Ureno ubingwa wa Dunia mwaka huu, kutokana na kuwa kwenye kiwango bora na hata jinsi alivyozianza fainali za mwaka huu lakini ikawa tofauti.
Moscow, Russia. Katika kile kinachoonekana kama angali na tamaa ya kutwaa ubingwa wa Dunia, mshambuliaji mahiri wa Ureno, Cristiano Ronaldo amekataa kuzungumzia suala la kustaafu soka la kimataifa.
Mshambuliaji huyo Real Madrid mwenye miaka 33 aliyetarajiwa kuipa Ureno ubingwa wa Dunia mwaka huu, kutokana na kuwa kwenye kiwango bora na hata jinsi alivyozianza fainali za mwaka huu lakini ikawa tofauti.
Licha ya kufunga mabao manne katika mechi za makundi na kufanikiwa kuipeleka Ureno hatua ya 16 bora, alishindwa kuibeba dhidi ya Uruguay na kujikuta ikitolewa kwa mabao 2-1.
Akijibu kwa mkato swali la mwandishi wa BBC, aliyetaka kujua iwapo atastaafu, Ronaldo alijibu kwa kifupi kuwa hawezi kuzungumzia lolote kwa sasa juu ya kustaafu, badala yake anahitaji kupewa muda wa kutafakari jinsi tulivyotolewa.
Mshambuliaji huyo aliyetwaa mara tano taji la mchezaji bora wa mwaka wa Dunia, ameshinda kila kitu akiwa na klabu, aidha ameanza kuonyesha mafanikio kwa taifa baada ya kuipa ubingwa wa Ulaya ‘Euro 2016’, anatamani kuipa Ureno ubingwa wa Dunia awe mshindi wa kila kitu katika soka.
Tayari Kocha wa Ureno, Fernando Santos, amesema atamshawishi nahodha wake huyo asistaafu ili acheze fainali zijazo za Kombe la Dunia itakazofanyika Qatar mwaka 2022, akisema Ronaldo atakua na miaka 37.
“Ninafuraha kwa kuweza kufika 16 bora, ingawa hayakua malengo yetu kuishia hapa lakini nadhani tumejitahidi, kikosi chetu kina vijana wengi ambao watakuwa tayari kushinda miaka minne ijayo, hata hivyo tutazungumza na Ronaldo ili aendelee kuwaongoza vijana,” alisema Santos.
Sio Ronaldo pekee bali hata hasimu wake wa kisoka Lionel Messi wa Argentina mwenye miaka 31, ambaye naye ameziaga fainali hizo baada ya kufungwa 4-3 na Ufaransa, hajazungumzia juu ya kustaafu.