Zidane: Kondoa nzima inaniangalia

Summary


DODOMA. MMOJA wa wachezaji wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara ni mshambuliaji kinda wa Dodoma Jiji, Zidane Sereri ambaye amekuwa kwenye kiwango cha juu sana msimu huu.

Kinda huyo ameaminiwa na Kocha Melis Medo kiasi cha kuanza katika kikosi cha kwanza mbele ya wachezaji wakongwe, Colins Opare, Hassan Mwaterema na Seif Karihe na amekuwa na kiwango bora licha ya umri mdogo alionao.

Mwanaspoti limefanya naye mahojiano kwa kina na kufunguka mambo kadhaa ikiwemo alivyojisikia mara baada ya kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu na wakongwe.

Haikuwa rahisi
Kinda huyo anasema ni kama bahati Mungu ameamua acheze Ligi Kuu kwani hakuwahi kuwaza kama inaweza kutokea akapata nafasi.

“Nilikuwa nacheza kwenye mashindano ya Umiseta na Umitashumta, sikuwahi kuwaza kama itakuwa rahisi namna hii ila nimepambana mpaka kufikia hapa jambo ambalo naona ni zuri sana kwangu."

Alivyopata nafasi
“Mimi ni mwenyeji wa Kondoa, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (Dorefa), Aden Mohammed alikuja Kondoa akaniona nacheza akavutiwa na uchezaji wangu.

“Akasema mimi nina kipaji kikubwa akanichukua akanileta Dodoma akanipeleka katika timu ya Makole Academy inayofundishwa na Kocha Omary Omarooh.
“Kocha Omarooh pia ni kocha wa timu ya vijana ya Dodoma Jiji U17 alivyoona nina kipaji akanichukua na kunipeleka timu ile ya vijana ya Dodoma Jiji.

“Nikiwa mazoezini akaja kocha wa timu ya wakubwa Masoud Djuma akafurahia uwezo wangu na akamwambia Omarooh ananitaka timu ya wakubwa.
“Sikulala siku hiyo, sikuamini nimepata nafasi ya kucheza timu ya wakubwa, nikaenda mazoezini na kocha alifurahi sana kuniona."

Mechi ya kwanza
Anasema baada ya kufanya mazoezi na timu na kuaminiwa Kocha Djuma alimhakikishia kumpa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza katika mchezo dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

“Huwezi kuamini Kocha Djuma akasema ananipa nafasi ya kucheza katika mchezo dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, mkoani Tanga msimu uliopita.
Anasema alitakiwa kucheza mchezo dhidi ya Yanga lakini leseni yake ilichelewa kuja hivyo ikabidi asubiri mchezo dhidi ya Coastal.

“Aliniambia nitakuanzisha hivyo sikuwa na wasiwasi sana hata wakati anatangaza kikosi kitakachoanza nilijua lazima nami nitakuwa mmoja wao.

“Aliwaambia wachezaji wenzangu ambao ni wakongwe wasinigombeze hata kama nitakosea, nilicheza vizuri sana ile mechi na kipindi cha pili nilitoka akaingia Hamis Mcha.

“Ninamshukuru Kocha Djuma kwa kuniamini, namshukuru Aden kwa kunitoa kijijini na Kocha Omarooh kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuweza kuonekana, popote mlipo nasema asanteni sana, Mungu awabariki na awape maisha marefu nafikiri ni kazi nzuri sana walifanya kwangu na wafanye kwa wengine,” anasema kinda huyo.
 

Malengo
Anasema malengo aliyojiwekea ni kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kama ilivyo kwa Kelvin John anaekipiga Genk ya Ubelgiji.

“Hata kama nitacheza Simba ama Yanga nataka kwenda mbele zaidi ili ndoto yangu iweze kutimia. Naamini itatimia, bado nina umri mdogo na nina kesho nyingi,” anasema kinda huyo anayemzimia msanii Ali Kiba.
Kinda huyo anasema wakati akiwa Kondoa alikuwa akipenda kumwangalia mshambuliaji wa Kagera Sugar, Anuary Jabir.

“Nampenda na ninamkubali sana na anajua nampenda na nilishamwambia nataka kucheza kama yeye.
“Nimekutana naye Dodoma Jiji lakini yeye aliondoka na kwenda Kagera Sugar, napenda jinsi anavyotunza mali na anavyotumia nguvu kupambana.

“Hata yeye aliniambia nacheza kama yeye, ila nina mwendo kuliko yeye, nafurahia kucheza naye na kila siku nawasiliana naye kwa njia ya simu tunazungumza mambo mengi,” anasema Sereri.

Kondoa nzima
Wachezaji wanaotoka wilayani Kondoa katika Ligi Kuu Bara ni pamoja na Abdul Majid Mangalo wa Singida Big Stars ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Itolwa.
Mwingine ni Sireri ambaye anasema anajivunia kutoka katika eneo hilo kwani kila mmoja anampa ushirikiano.

“Nikiwa nacheza Kondoa nzima inaniangalia, najivunia kuwa mzaliwa wa Kondoa kwa sababu kule ndiko wazazi wangu na marafiki zangu wapo,” anasema.

Bao la kwanza
Ilikuwa katika mchezo dhidi ya Mbeya City na alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Hassan Mwaterema.
“Msimu uliopita sikupata nafasi ya kufunga, niliweka dhamira lazima msimu huu nifunge na kweli kocha mpya Melis Medo alionyesha kuniamini kwa kiwango kikubwa.

“Akanianzisha katika mchezo dhidi ya Mbeya City niliocheza kwa dakika 90 na tulishinda mabao 2-1 na mimi ndio nilifunga bao la ushindi.

“Inabaki kuwa kumbukumbu ambayo haitafutika katika maisha yangu ndio maana nilipofunga nilishindwa kuelewa nikimbilie wapi sikuamini kwa sababu niliona haya ni zaidi ya maajabu."

Zidane halisi
“Hili ni jina langu la asili sio la bandia, baba yangu Omary Sereri alikuwa mchezaji wa soka na aliichezea timu ya Halmashauri ya Kondoa.

“Hakufanikiwa kucheza sana soka la ushindani, lakini alikuwa akimpenda sana Zinedine Zidane wa Real Madrid, hivyo aliamua kunipa jina hilo.

“Jina hili naamini limekuwa baraka kubwa kwangu kwa sababu kila mmoja anajua uwezo wa Zidane katika soka pamoja na uwezo wake wa kufundisha,” anasema.
Akizungumzia juu ya kuongezwa kwa mshambuliaji mwenye uzoefu Steven Sey ambaye amewahi kuichezea Namungo anayeungana na kina Collins Opare, Hassan Mwaterema, Seif Karihe, Christian Zigar na Paul Peter, Zidane anasema;

“Nikiri ushindani ni mkubwa kwangu, hiyo ni chachu ya kuendelea kujituma na kila siku napambana kumwaminisha Kocha Medo naweza,” anasema.

City yamzibua
“Mwaka 2020 nikiwa Kondoa, Mbeya City ikiwa inatokea Dodoma ikaomba mchezo wa kirafiki na kombaini ya Kondoa.
“Nikiwa nimejipumzisha nyumbani viongozi wa chama cha Soka Kondoa walinipigia simu wakinitaka siku inayofuata nikacheze mchezo wa kirafiki dhidi ya Mbeya City.

“Nilishtuka sana na nikaingia uoga kutokana na umri wangu na kwa jinsi nilivyokuwa nikiifahamu Mbeya City.
“Nikaenda kucheza mchezo ule na nilionesha uwezo mkubwa sana na Kocha wa Mbeya City wakati huo, Amri Said alichukua namba zangu akasema atanitafuta na atanisajili katika dirisha dogo.

“Niliporudi nyumbani niliwaza vitu vingi sana nikaamini najua na naweza kucheza mpira kama nimewasumbua Mbeya City tena timu ya Ligi Kuu basi  nina uwezo wa kucheza timu yoyote.

“Baada ya hapo, nikaja kuchukuliwa na kuja Dodoma lakini niliamini baada ya mechi ile mimi naweza na nitafika mbali,” anasema Sireri.
Anasema katika vitu ambavyo vinamkuza kila siku ni uwezo wa kucheza na  mabeki wa Dodoma Jiji wenye maumbo makubwa.

“Kila siku mazoezini nakabana na Nsata (Augustino), Bilaly (Justin), Ninja (Abdallah Shaibu) wakati yupo Dodoma Jiji kwa mkopo akitokea Yanga, Kibacha (Mbwana), Kalambo (Aron) wana maumbo makubwa.
“Lakini hata wao wanafurahi kucheza na mimi kwa sababu wanasema nawaongezea kitu kwa sababu ya kasi yangu,” anasema kinda huyo.
 

Ligi bara ilivyo
“Ni ngumu sana, mzunguko wa kwanza mwishoni tulijitahidi tukatoka mkiani, lakini hali bado ni ngumu kwetu tunatakiwa kupambana.

“Kubwa tumemaliza michezo na timu kubwa sasa tunatakiwa kujipanga kupata ushindi ili tuendelee kubaki katika ligi,” anasema mchezaji huyo anayehusudu wali maharage.