Prime
Yanga yala sahani moja na Waarabu
WABABE wa soka nchini, Yanga imetolewa katika michuano ya CAF baada ya kuzidiwa ujanja na Al Ahly ya Misri iliyoongoza Kundi B na As FAR Rabat ya Morocco iliyoshika nafasi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hilo haijaifanya isiendelee kutunishiana misuli na timu za Kiarabu.
Yanga ilimaliza ikiwa ni ya tatu katika kundi hilo licha ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, kwani sare isiyo na mabao ya Al Ahly na Sa FAR iliikwamisha kwa pointi nane ilizokusanya dhidi ya ilizokuwa nayo wapinzani wao hao.
Al Ahly ilikuwa na 10, AS FAR yenyewe ilimaliza na tisa, huku JS Kabylie ikiganda mkiani mwa kundi na pointi mbili tu.
Hata hivyo, Yanga imeendelea kuwa klabu ya Afrika Mashariki inayobanana na Waarabu kwa kuongoza orodha ya timu zilizotwaa mataji mengi ya Ligi za soka Afrika, ikiwa ndani ya 10 Bora, huku watani zao Simba wakiwa nafasi ya 11 katika timu zenye mtaji mengi ya Ligi Kuu.
Kwa mujibu wa takwimu zilipo kwa sasa ni klabu ya Al Ahly ya Misri ndiyo inayoongoza Afrika kwa kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu ikiwa na 45, lakini ndio inaoongoza duniani kwa sasa kwa mataji mengi zaidi tofauti nje ya ligi ikifuatiwa na Real Madrid ya Hispania.
Wababe hao wa Misri walianza kubeba taji la ligi Misri mara ligi hiyo ilipoasisiwa Oktoba 22, 1948 kwa kubeba msimu wa kwanza wa 1948-49 na kukusanya kwa misimu kadhaa wa mwisho ikiwa ni msimu uliopita wa 2024-2025, ilipoipiku Pyramids iliyoonekana kama ingebeba taji.
Klabu ya pili kwa kubeba mataji mengi Ligi Kuu kwa Afrika ni Esperance ya Tunisia yenye mataji 34 ikianza kubeba tangu mwaka 1942 katika ligi hiyo iliyoasisiwa rasmi Juni 9, 1907, huku taji la mwisho ililitwaa msimu uliopita wa 2024-2025.
Yanga ya Tanzania, St George ya Ethiopia na Al Hilal ya Sudan ambazo zote zinatokea Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ndizo zinazoshika nafasi ya tatu kwa pamoja, kila moja ikitwaa jumla ya mataji 31 ya ligi katika nchini zao.
Al Hilal ya Sudan ambayo kwa sasa inashiriki Ligi Kuu ya Rwanda kutokana na Sudan kuwa na machafuko ya kisiasa katika orodha hiyo ndio inayofuata ikiwa na mataji hayo 31 ilichukua kuanzia 1965 ilipoasisiwa ligi ya nchini humo hadi msimu uliopita ikiwa inashiriki Ligi Kuu ya Mauritania.
Yanga ipo nyuma ya Al Hilal katika orodha hiyo ya timu zilizobeba mataji mengi ya Ligi Afrika, yenyewe katika mataji 31 iliyochukua ya Ligi ya Bara iliyoasisiwa 1965, ilianza kubeba kuanzia 1968 hadi msimu uliopita wa 2024-2025 ikilishikilia kwa misimu minne mfululizo tangu 2021-2022.
St George katika mataji ya Ligi Kuu ya Ethiopia iliyoasisiwa mwaka 1944, ilianza kubeba kuanzia 1950 na mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2023 ikifunga hesabu ya tano bora kwa klabe zenye mataji mengi, huku Asec Mimosas ya Ivory Coast ikiwa nyuma wa wababe hao wa kutoka CECAFA.
Asec Mimosas yenyewe imetwaa mataji 29 katika Ligi ya Ivory Coast iliyoanzishwa mwaka 1960, ikifutiwa kwa mbali na Asante Kotoko ya Ghana yenye mataji 25 ya Ligi ya nchi hiyo iliyoasisiwa tangu 1958, wakati Djoliba ya Mali ikifuata katika orodha hiyo kwa mataji 24 iliyotwaa katika Ligi ya nchi hiyo iliyonzishwa mwaka 1966.
Klabu mbili zinazokamilisha idadi ya klabu 10 Bora zilizobeba mataji mengi ya Ligi inashikiliwa na APR ya Rwanda iliyotwaa 23 katika ligi iliyoasisiwa mwaka 1969, huku Wydad ikifunga hesabu ikiwa na 22 sawa na iliyonayo Simba ya Tanzania, lakini yenyewe imebeba taji la mwisho msimu wa 2021-2022 baada ya kubeba la kwanza msimu wa 1947-1948 katika ligi iliyoazisiwa Juni 11, 1915.
Licha ya kuwa katika Tano Bora ya wababe wa Ligi Kuu za Afrika, lakini Yanga ni moja ua klabu zilizobeba mataji mengi kwa ujumla tofauti, ikiwa na 62, ilihali Al Ahly ikiongoza na mataji 157, yakiwamo 45 za Ligi, 39 ya Kombe la FA, 16 ya Egypt Super Cup na 12 ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia imebeba Kombe la Washindi Afrika mara nne, CAF Super Cup (8), Sultan Hussein Cup (7), Cairo League (17), Kombe la Shirikisho Afrika (1) na mataji mengine lukuki naa kutisha Afrika na duniani.