Yanga ya Zahera inahitaji uelekeo huu

Muktasari:
- Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ni kama Yanga imeshachemka na sasa inabidi igeukie michuano mingine iliyo mbele yao hasa Ligi Kuu Bara.
YANGA juzi usiku ilicheza mchezo wake wa nne wa ukiwa ni warudiano dhidi ya Gor Mahia ya Kenya. Katika mchgezo huo, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Gor Mahia na kufuta matumaini yao ya kusongo kutoka hatua ya Makundi iliko sasa.
Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ni kama Yanga imeshachemka na sasa inabidi igeukie michuano mingine iliyo mbele yao hasa Ligi Kuu Bara.
Ni wazi Yanga inahitaji kurudisha makali yake na Kocha wake, Mwinyi Zahera ana kazi ya kusuka upya kikosi hicho hasa baada ya usajili ili kuweza kupata matokeo katia michuano mbalimbali hasa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Safu ya ushambuliaji
Kocha Zahera ana kibarua kigumu cha kuhakikisha anakisuka vizuri kikosi chake hasa safu ya ushambuliaji itakayomzalia mabao msimu mpya utakapoanza. .
Zahera ana washambuliaji ambao ni Matteo Anthony, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Ibrahim Ajib, Yusuph Mhilu, Yahya Akilimali, Said Mussa, Yohana Mkomola na Heritier Makambo, akifanikiwa kuunda kombinesheni zao zinaweza kumbeba katika ligi ijayo.
Safu hiyo imefunga mabao matatu tu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika inayoendelea, huku safu ya ulinzi ikiruhusu mabao tisa, hilo linadhihirisha Kocha Zahera bado ana kazi ya kutengeza kisawasawa kikosi chake.
Safu ya ulinzi
Mbali na safu ya ushambuliaji kuwa butu, Kocha Zahera bado atakuwa na kazi ya ziada kuinoa upya safu ya ulinzi kuhakikisha inafanya kazi yao kikamilifu, tofauti na namna ilivyoweza kuruhusu mabao mengi katika michuano ya Shirikisho Afrika.
Ingawa safu hiyo haijabadilika sana kwani bado wapo wachezaji ambao wamecheza pamoja muda mrefu kama beki ya kati Kelvin Yondan na Andrew Vicent ‘Dante’, beki namba mbili kuna Juma Abdul na Haji Mwinyi na Gadiel Michael ambao wana uzoefu, kikubwa Kocha Zahera ni kuwajengea morali ya kutosha.
Kauli za wachambuzi
Ally Mayay ni winga wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka nchini, alisema tatizo kubwa analoliona kwa wachezaji wa timu hiyo ni kuathirika kisaikolojia kutokana na kipindi cha mpito cha kuyumba kwa uchumi ndani ya klabu hiyo.
“Wachezaji waliopo sio wabaya, wanatakiwa kuikubali hali wanayoipitia haitadumu milele, wajitume kwa bidii kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri, naamini hata katika ligi watafanya kitu cha tofauti.
Wakati aliyekuwa katibu wa timu hiyo na mchezaji wa zamani Lawrence Mwalusako alisema Kocha Zehera anatakiwa kuweka sawa akili za wachezaji ndipo aendelee na programu yake ya maandalizi ya msimu mpya.
“Maandalizi ya mchezaji yanaanzia kwenye akili ndipo mwili unakuwa tayari kufanya kazi kikamilifu, wachezaji wameathiriwa na mtikisiko wa kiuchumi, wanawaza mwisho wao ni nini, lakini hiyo ni Yanga itakaa vizuri na watakuwa imara katika ndoto zao,” alisema.
Kauli za wachezaji
Mshambuliaji wa timu hiyo, Matteo Anthony alisema kitu pekee alichokigundua kinawagharimu ni hali ya kucheza kitimu imepotea, imebakia kila mchezaji kujaribu kupambana.
“Tumepoteza hali ya kucheza kitimu bila shaka naamini kocha atakuwa ameliona hilo, tutajitahidi kupambana kwa kadri tuwezavyo ili kumaliza kwa ushindi katika mechi mbili zilizosalia dhidi USM Alger na Rayon Sport.
“Niweke wazi hali tunayopitia kwa sasa, haimanishi katika ligi tutafanya ovyo, haya yanapita, tutafanya vizuri mashabiki wasichoke kutuunga mkono katika hali zote,” alisema.
Naye Haji Mwinyi alisema bado wanaamini katika kufanya vizuri na kuacha upepo wa kila namna upite, huku wakiendelea kujiweka fiti kwa ajili ya ligi.
“Kila kazi ina changamoto zake ama katika maisha ya mtu yoyote ana wakati wa furaha na huzuni, kufanya vibaya kwetu hakumaanishi haitakaa itokee tukafanya vizuri, tukutane kwenye ligi kwani soka linachezwa uwanjani na si kelele,” alisema.